DK SALIM AZINDUA KAZI ZA PROFESA HAROUB OTHMAN

Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Afrika (AU), Dk. Salim Ahmed Salim amesema kuwa mwanazuoni maarufu marehemu Profesa Haroub Othman alikuwa muumini wa Muungano wa serikali mbili.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu cha mkusanyiko wa kazi za Othman, Salim alisema msimamo wake kuhusu muungano ulikuwa wazi na tofauti na watu wanavyoelezea.
“Haroub (Othman) alikuwa akiona fahari kuwa Mtanzania na kamwe hakuidharau Zanzibar, alikuwa muumini wa muungano wa serikali mbili,” alisema.
Akizungumza kitabu hicho, Mke wa Marehemu Othman, Profesa Saida Yahya Othman alisema kitabu hicho chenye jina la ‘Yes in My Lifetime’ kinajumuisha makusanyo ya hotuba, makala na mihadhara aliyotoa wakati wa uhai wake kuanzia mwaka 1974 hadi mwaka 2009.
Alisema makala zilizomo ndani ya kitabu zinazungumzia mapambano dhidi ya ubeberu, kupitia mshikamano wa wapigania haki za wanyonge kote duniani na muungano wa Tanzania.
“ Kitabu hiki ni muhimu katika jamii yetu ambamo historia inakuwa kama ukoma, tunafikiri ukombozi wetu utakuja kwa kuwaiga wengine bila ya kuhoji,  tunafikiri utaifa ni chuki dhidi ya waliokuwa tofauti na sisi na uzalendo uchwara,"alisema.
Othman alifariki dunia miaka mitano iliyopita, alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria cha Zanzibar na mjumbe wa Baraza la Habari la Tanzania(MCT).

No comments: