DC AAGIZA KUKAMATWA WAGANGA WA JADI WANAOSAIDIA WAJAWAZITO



Mkuu wa Wilaya Kibondo, Venance Mwamotto ametoa agizo kukamatwa kwa waganga wa kienyeji wanaowapa wajawazito dawa za kuwasaidia kujifungua.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema kwamba vitendo hivyo vinasababisha kuendelea kwa vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga kwa kushindwa kuhudhuria kliniki na kujifungulia kwenye vituo vya afya. 
Mwamotto alisema hayo mjini Kibondo wakati wa kampeni ya uhamasishaji jamii kujitolea damu kwa hiari iliyokuwa ikiendeshwa na  Taasisi ya Evidence for Action kupitia kampeni yake inayojulikana kama Mama Ye. 
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa kwa muda mrefu sasa licha ya uhamasishaji unaofanywa kwa jamii ili kuwapeleka akinamama wajawazito kujifungua hospitali na vituo vya afya bado jamii imekuwa ikiendelea kuwatumia waganga wa jadi hali ambayo imechangia vifo vya akinamama hao. 
“Tumehamasisha kwa maneno kwa jamii kuwahimiza mama wajawazito kujifungulia katika vituo rasmi vya kutoa huduma lakini bado wengi wanaenda kwa waganga wa kienyeji, agizo kuanzia sasa waganga wa kienyeji watakaoendelea kuwahudumia na kutoa dawa kwa mama wajawazito badala ya kuwapeleka hospitali tutawakamata na kuwachukulia hatua,” alisema Mwamotto. 
Awali Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Emanuel Mwasulama alisema kuwa licha ya maboresho makubwa ya miundo mbinu ya utoaji huduma yaliyofanywa na Shirika la World Lung Foundation katika vituo vya utoaji huduma wilayani humo bado vifo vya akinamama wajawazito na watoto wachanga vimeendelea kutokana na wajawazito  kujifungulia nyumbani na kuchelewa kuhudhuria kwenye vituo vya afya na zahanati. 
Wakati huo huo viongozi wa Serikali ya Kijiji, wahudumu wa afya na wananchi wa Tarafa ya Nguruka katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma wamelalamikia kutokuwepo kwa friji maalumu la kuhifadhia damu kwenye kituo cha afya Nguruka hali inayofanya wananchi kukatishwa tamaa na uchangiaji damu kwa hiari. 
Walisema hayo wakizungumza na timu ya waandishi wa habari iliyofanya ziara katika kituo hicho kuona hali ya udhibiti wa vifo vya akinamama wajawazito na watoto kufuatia uboreshaji wa miundombinu ya utoaji huduma na ujenzi wa chumba cha upasuaji uliofanywa na shirika la World Lung Foundation. 
Akizungumza jambo hilo Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Beatrice Mtesigwa alisema kuwa kuboreshwa kwa kituo hicho na kujengwa kwa chumba kidogo cha upasuaji kumechangia kuwafanya akina mama wajawazito kuongezeka maradufu katika kufuata huduma na kujifungua kwenye kituo hicho.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Kijiji cha Nguruka, Yakubu Mussa Nzigamiye amesema kuwa licha ya kuboreshwa kwa kituo hicho cha afya na kujengwa kwa chumba cha upasuaji wanachangamoto kubwa ya kutokuwepo kwa chumba cha kuhifadhia damu hali ambayo inalazimu kutokuwepo kwa damu ya akiba.

No comments: