DAWASCO YAELEZA CHANZO CHA SHIDA YA MAJI DAR

Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasco), limesema tatizo la maji katika baadhi ya maeneo jijini limetokana na kuzimwa kwa mitambo pamoja na kupasuka kwa bomba la maji  Ruvu Chini.
Ofisa Mtendaji wa Dawasco, Jackson Midala aliliambia HabariLeo jana kuwa hata hivyo bomba lililopasuka limeshatengenezwa na kukamilika tangu jana.
Kuhusu maeneo mengine yanayokosa maji kama Kimara na Ubungo alisema maeneo hayo hupata maji kulingana na mgao.
Alisema Dar es Salaam ipo katika mpango wa kupata maji ya uhakika na kwamba bomba la Ruvu Chini limekamilika na litakuwa likipitisha maji lita milioni 270 kwa siku.
Alisema kinachosubiriwa kwa sasa ni mtambo mpya wenye kuunganisha bomba lililoishia eneo la Tegeta kuja Dar es Salaam linalotarajiwa kukamilika mwishoni mwa Julai mwaka huu.
Kuhusu Ruvu juu alisema mkandarasi yupo katika eneo la kazi na ifikapo Septemba mwakani wakazi wa Kibaha, Mlandizi, Mbezi na Kimara watapata maji ya kutosha.
Hata hivyo alisema mpango wa maji ya uhakika Dar es Salaam ulishindwa kukamilishwa kwa wakati Januari mwaka huu kutokana na wananchi wengi kufungua kesi mahakamani.

1 comment:

Anonymous said...

Hali ya kukosekana kwa maji takriban wiki moja sasa ni mbaya sana kiasi kwamba watu wamekosa imani na DAWASA hii ni kwa sababu hawatoi taarifa ya walipofikia na ni lini maji hayo yatatoka kwa uhakika. kweli wenye watoto na vyoo vya kuflush tunateseka. Harun mkazi wa Ilala