BAJETI KUU YA MATRILIONI YASUBIRIWA KWA HAMU



Bunge linaendelea na mkutano wake wa 15 mjini Dodoma leo, huku shughuli kubwa wiki hii ikiwa ni kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali ya matrilioni ya shilingi.
Bajeti hiyo ni ya mwaka wa fedha 2014/15. Pia, wiki hii kutafanyika uchaguzi wa wawakilishi wa Bunge katika taasisi mbalimbali.
Kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali, Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya alieleza Aprili 30, mwaka huu kuwa Serikali imepanga kutumia Sh trilioni 19.7 katika mwaka wa fedha wa 2014/15 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shughuli za maendeleo.
Mkuya alisema hayo jijini Dar es Salam, wakati akiwasilisha Mpango wa Bajeti ya mwaka ujao wa fedha kwa wabunge.
Alisema kati ya fedha hizo, fedha za matumizi ya kawaida ni Sh trilioni 14.2 na zilizosalia ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Waziri wa Fedha alisema katika matumizi ya maendeleo, Serikali imeweka kipaumbele katika maeneo sita ya kilimo, elimu, maji, nishati,  utafutaji rasilimali fedha na uchukuzi ikiwemo reli, barabara, madaraja, magati, bandari, usafiri wa majini na usafiri wa anga.
Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, Waziri wa Fedha atasoma Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali Juni 12, mwaka huu saa 10:00 jioni; na siku inayofuata pamoja na siku za mwisho wa wiki, wabunge  watasoma na kutafakari hotuba hiyo.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, mjadala kuhusu bajeti hiyo, utachukua siku saba, ambapo utaanza Juni 16 hadi Juni 24, mwaka huu.
Bajeti ya sasa utekelezaji wake unaishia Juni 30, mwaka huu, ambapo Serikali ilipanga kutumia Sh trilioni 18.2. Tayari Serikali imekutana na baadhi ya washirika wa maendeleo kwa siku mbili mjini hapa, kwa lengo la kuwataka waeleze utekelezaji  wa ahadi zao za kuchangia bajeti ya Serikali, kwa mwaka unaoishia Juni 30, mwaka huu. Nchi ya Japan imeshatangaza kuwa itatekeleza ahadi yake.
“Tutakuwa na mkutano washirika wa maendeleo hapa Dodoma kwa siku mbili kuanzia kesho. Tutajadiliana na kuwaomba wakamilishe ahadi zao kabla ya  tarehe 30 Juni mwaka huu,” alisema Waziri wa Fedha, bungeni  Alhamisi iliyopita.
Mkuya aliahidi kuwa wizara yake, itatafuta fedha kutoka katika mafungu na vyanzo vingine ili kuzipeleka katika wizara ambazo zilipata fedha pungufu ya zile zilizoidhinishwa bunge mwaka jana.
Baadhi ya wizara hizo ni Nishati na Madini, Maji, Uchukuzi, Afya na Ustawi wa Jamii na Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Baadhi ya wizara hizo zimepata kati ya asilimia 20 na asilimia 30 ya fedha zilizoidhinishwa mpaka kufikia Aprili mwaka huu, ikiwa imesalia miezi miwili kumalizika kwa mwaka wa sasa wa fedha.
Kwa mfano, hadi kufikia Aprili  mwaka huu, Serikali ilikuwa imeipatia Wizara ya Maji Sh bilioni 39.4 tu zilizoidhinishwa na bunge. Fedha hizo ni sawa na asilimia 28 tu ya kiasi kilichoidhinishwa. Fedha hizo pia ni sawa na upungufu
wa Sh bilioni 98.9.
Serikali inatazama upya bajeti za wizara zote ili kutafuta vyanzo vingine vya fedha  za kupeleka katika wizara, ambazo bajeti zake zina upungufu.
Kinachofanyika sasa ni Serikali kupata karibu Sh trilioni 1.8 ambazo zimepungua katika bajeti kuu ya mwaka jana ya Sh trilioni 18.2.
Kuhusu maandalizi ya Bajeti ya 2014/15, tayari Serikali
imeanza kufanya mashauriano ya siku sita na Kamati ya Bunge ya Bajeti, inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Lengo la mashauriano hayo ni kufanya majumuisho na kuzingatia hoja zenye maslahi ya Taifa, zilizojitokeza wakati wa kujadili bajeti za wizara moja moja.  Majadiliano hayo yanahudhuriwa pia na wenyeviti wa Kamati zote za Kudumu za Bunge.
 Kwa upande wa uchaguzi wa wawakilishi wa Bunge, kwa mujibu wa Naibu Spika, Job Ndugai,  tarehe ya mwisho ya kurejesha fomu kwa wanaotaka kugombea ni Juni 8, mwaka huu saa 10:00 jioni.
 “Nawatangazieni chaguzi mbalimbali zitakazofanyika. Wale ambao mtapenda kushiriki, chukueni fomu kwa Katibu wa Bunge kuanzia Juni 4 hadi Juni 8, mwaka huu saa 10,00 jioni,” alisema Naibu Spika, Job Ndugai Juni 4, mwaka huu alipotoa matangazo bungeni.
Nafasi hizo za uwakilishi ni kundi la kwanza ni wajumbe wa Bodi ya Mabaraza ya Vyuo Vikuu. Vyuo vikuu vya Serikali ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu Mzumbe (MU),  Chuo Kikuu Cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Chuo Kikuu Cha Mbeya cha Sayansi na Teknolojia (MIST).
Ndugai alisema Kundi  la pili ni Mwakilishi wa Bunge katika mabunge ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Nafasi ipo wazi kutokana na aliyekuwa mwakilishi, Dk Titus Kamani kuteuliwa na Rais hivi karibuni kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Kundi lingine ni Mwakilishi katika Tume ya Utumishi wa Bunge, kutokana na aliyekuwepo, Godfrey Zambi kuteuliwa na Rais hivi karibuni kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.

No comments: