Watanzania
leo wanaelekeza macho na masikio yao mjini Dodoma, kusikiliza Hotuba ya Bajeti
ya Serikali, inayotarajiwa kusomwa saa 10 kamili bungeni na Waziri wa Fedha,
Saada Mkuya Salum.
Tayari
Waziri Saada alishaeleza kuwa makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa
fedha wa 2014/15, unaoanza Julai mwaka huu, yatakuwa Sh trilioni 19.6 kutoka
makadirio ya Sh trilioni 18.2 ya Bajeti inayoisha muda wake.
Vipaumbele
vya Bajeti hiyo, kwa maana ya miradi itakayozingatiwa zaidi, ni iliyo katika
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) unaohusisha sekta sita za Kilimo, Elimu,
Maji, Utafutaji rasilimali fedha, Nishati, Uchukuzi na Uboreshaji wa Mazingira
ya kufanyia biashara na Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano.
Akisoma
mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2014/2015, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, alisema mapendekezo ya mpango huo,
yana vipaumbele vitano.
Cha
kwanza ni miundombinu, kikifuatiwa na kilimo, viwanda vinavyotumia malighafi za
ndani na kuongeza thamani, maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi na uendelezaji
wa shughuli za utalii, biashara na fedha.
Katika
hotuba hiyo, Watanzania wengi watakuwa makini kusikiliza bidhaa na huduma
zitakazoongezwa kodi, jambo linalotarajiwa kuongeza bei ya bidhaa za huduma
husika katika soko.
Katika
bajeti inayoishia, Serikali iliongeza
kodi kwenye magari makuukuu, bia, vinywaji vikali na baridi ambavyo kodi
imekuwa ikiongezwa kila mwaka na kuwaathiri watumiaji.
Kutokana
na hali hiyo wanywaji pombe na sigara baada ya bajeti ya mwaka juzi ya
2012/2013, walilazimika kutumia fedha nyingi ili kupata huduma hizo kwa kiwango
kile kile katika mwaka huu wa bajeti unaoisha.
Bidhaa
zisizokuwa za mafuta ambazo zilifanyiwa marekebisho na kuongezwa kodi ni
mvinyo, pombe, vinywaji vikali, na sigara.
Ushuru
pia uliongezwa kwenye magari yasiyokuwa ya uzalishaji na yenye umri wa miaka 10
kutoka asilimia 20 mpaka asilimia 25.
Lengo
la Serikali katika hilo, lilikuwa kupunguza uagizaji wa magari chakavu ili
kulinda mazingira na kupunguza ajali za mara kwa mara.
Katika
bajeti hiyo, vijana wa bodaboda walicheka baada ya Serikali kusamehe ushuru wa
barabara kwa pikipiki hizo za biashara.
Moja
ya kivutio kikubwa cha Bajeti inayowasilishwa leo, ni matarajio ya wafanyakazi
kuhusu utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa katika sherehe za
Mei Mosi mwaka huu, ya kuongeza mshahara wa kima cha chini na kupunguza kodi ya
mshahara (PAYE).
Rais
Kikwete alisema Serikali itaendelea kuongeza mshahara wa kima cha chini na
kubainisha kuwa mwaka 2005 alipoingia madarakani, alikuta mshahara wa kima cha
chini ni Sh 65,000 na kukipandisha taratibu hadi kufikia Sh 240,000 cha sasa.
Kuhusu
kupunguza PAYE, Rais Kikwete alisema kusudi la Serikali ni kupunguza kodi hiyo
ya mshahara kutoka asilimia 13 inayotozwa sasa, ifikie katika kiwango cha
tarakimu moja.
Kuhusu
misamaha ya kodi ambayo mwaka huu imekuwa gumzo bungeni, huku wabunge wengi
wakitaka ipunguzwe, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alinukuliwa akisema
wafanyabiashara na vigogo wanaokwepa kodi kwa kujificha kwenye mwavuli wa
misahama, hawako salama.
“Tutafuatilia kikamilifu kwa kuwa wapo watu
wanaingiza bidhaa wanapewa msamaha, lakini ukija kwenye huduma za jamii unakuta
bidhaa hizo zinauzwa kibiashara,” alisema.
Mbali na kuondoa misamaha ya kodi, pia makusanyo ya ndani yatatiliwa mkazo zaidi ili kujenga uwezo wa kujitegemea wenyewe badala ya kutegemea wahisani.
Alisema eneo hilo ni muhimu mbalo Serikali inaona kuna haja ya kulisimamia vizuri, ili kuhakikisha fedha za wananchi zinatumika vizuri.
No comments:
Post a Comment