ATCL YAINGIA MKATABA NA KAMPUNI YA AFRIKA KUSINI

Kampuni ya Ndege ya Tanzania(ATCL) imesaini mkataba wa ushirikiano na kampuni ya Interair ya Afrika Kusini, itakayowezesha kampuni hiyo kuwa na safari tatu kwa wiki kati ya Dar es Salaam na Johannesburg, Afrika ya Kusini ikiwa ni kama ratiba ya mwanzo.
Taarifa hiyo imetolewa siku chache baada ya kampuni hizo mbili kusaini makubaliano ya kufungua soko la kitanzania kwa Interair na kulifufua soko la Afrika ya Kusini kwa ATCL kwa kupitia safari zitakazofanyika siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa, ikiwezeshwa na ushirikiano huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATCL, Milton Lazaro alisema ushirikiano huo na Interair ni sehemu ya mkakati wa kuboresha ATCL, kama siyo kwa safari za moja kwa moja basi kupitia ushirikiano wa aina hiyo, ili kuweza kurejesha huduma za kampuni hiyo katika njia zote ilizokuwa ikiruka, ikianzia Afrika ya Kusini. 
 “Kwa kutumia ndege za Interair, abiria wetu sasa watakuwa na uwezo wa kusafiri kwenda na kutoka Johannesburg katika siku zifuatazo; itawasili jijini Dar es Salaam kila Jumatatu na kuondoka kwenda Johannesburg Jumanne, kuwasili Dar es Salaam Jumatano na kuondoka siku hiyo hiyo, kuwasili Dar es Salaam Ijumaa na kuondoka kwenda Johannesburg siku ya Jumamosi,” alisema
Lazaro alibainisha kuwa kampuni hizo mbili sasa zinatoa fursa kwa wasafiri kutoka nchi hizo mbili kuyafikia masoko, wanaotaka kutumia na kupata uzoefu wa siku kuu za kipekee wanazokuwa wakizisoma kuhusu Afrika ya Kusini au Tanzania, na pia kutoa fursa za ongezeko la ushirikiano wa kibiashara na kidiplomasia.
Aliongeza kuwa ATCL katika siku za mbele itatanua safari zake mpaka Arusha, Zanzibar, Mwanza, Mbeya, visiwa vya Comoro na baadaye katika maeneo mengine yote inayofanyia shughuli zake.
Kwa upande wake, Meneja Interair wa Kanda ya Afrika Mashariki, Angelo Cossi, alisema: “Ushirikiano na ATCL ni muungano nzuri kwa sababu ya faida itakayopatikana ambayo itafaidisha kampuni hizi mbili.”
Alisema Interair ambayo ina makao yake makuu Johannesburg, Afrika ya Kusini, kwa sasa ina ndege aina za Boeing 727, 737 na 767, ambazo zinatoa huduma ndani ya Afrika na katika visiwa vya Bahari ya Hindi.

No comments: