ZANZIBAR YATANGAZA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 707.8


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetangaza Bajeti yake ya Sh bilioni 707.8, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ambayo imeweka kipaumbele zaidi katika kukusanya kodi na kutekeleza miradi ya maendeleo ya sekta ya miundo mbinu, elimu na afya.
Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee, alisema hayo wakati akitangaza Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014-2015 katika Baraza la Wawakilishi mjini hapa.
Mzee alitaja muelekeo wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ni kuimarisha mapato ya ndani na kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje ya nchi.
Alisema katika bajeti hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajiwa kukusanya  Sh bilioni 707.8, sawa na ongezeko la asilimia 7.5 ya makadirio ya bajeti ya mwaka 2013-2014 ya Sh bilioni 685 Bilioni.
Mzee alisema Sh bilioni 365.8 zinatarajiwa kukusanywa katika mapato ya ndani katika mwaka 2014/2015 ikilinganishwa na mapato ya mwaka 2012/2013 ya Sh bilioni 326.
Alisema serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imeweka mikakati ya kukusanya mapato zaidi katika vianzio vyake mbali mbali kupitia taasisi zake za kukusanya mapato TRA na ZRB.
Kwa mfano, alisema mamlaka ya mapato nchini (TRA) inakadiriwa kukusanya jumla ya Sh bilioni 166.1  sawa na asilimia 25.7 ya mapato halisi yaliyokusanywa katika mwaka 2013-2014. ya Sh bilioni 132.1.
Aidha Mzee aliwaambia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba mishahara ya watumishi wa Zanzibar inachukuwa asilimia kubwa ya mapato yote yanayokusanywa na serikali kwa asilimia 55.2.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitarajii kuongeza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wake, isipokuwa itafanya marekebisho ya mishahara kwa kada mbali mbali.
Mzee alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2014-2015 serikali itaongeza ada ya usalama wa anga kwa ajili ya kuimarisha mamlaka ya viwanja vya ndege nchini, ZAA.
Aidha alisema mamlaka mbili zinazokusanya mapato nchini ZRB na TRA zipo katika mchakato wa kuwatambua walipa kodi wote kuona kwamba wanalipa mapato ipasavyo katika taasisi husika.
Katika mwaka wa fedha 2014-2015 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajiwa kutumia jumla ya Sh bilioni 707.8  ambapo kati yake matumizi ya kawaida ni Sh bilioni 376.5  na Sh bilioni 331.3 ni kwa ajili ya mpango wa maendeleo.
Mapema Mzee alisema hadi kufikiya Machi 2014 deni la taifa limeongezeka hadi kufikiya Sh bilioni  294.90 sawa na ongezeko la asilimia 17.0 ikilinganishwa na deni la Sh bilioni 252.3 ilipofika Machi mwaka 2013.
Hata hivyo, Mzee alisema asilimia 88 ya deni la nje limedhaminiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na asilimia 12 limedhaminiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

No comments: