ZANTEL YAPAMBANA NA MALARIA SEHEMU YA KAZI

Kampuni ya simu za mkononi ya Zantel imegawa vyandarua zaidi ya 600 kwa wafanyakazi wake katika harakati za kupiga vita malaria sehemu za kazi.
Hatua hiyo inaendeleza mkakati wa Malaria Safe Initiative, ulioasisiwa na programu ya United Against Malaria (UAM), ukilenga kuhamasisha sekta binafsi kupambana na malaria katika maeneo ya kazi.
Mkakati huu unatekelezwa barani Afrika na Tanzania imekuwa ikifanya vyema, kwa kuwa na kampuni nyingi zilizo katika mkakati huo kupitia mpango wa Malaria Safe Companies. 
Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Pratap Ghose akizungumza wakati wa ugawaji wa vyandarua hivyo Dar es Salaam, jana, aliwasihi wafanyakazi hao kutumia vyandarua hivyo, inavyopasa kupambana na ugonjwa huo hatari.
Kwa upande wake, Ofisa Rasilimaliwatu wa kampuni hiyo, Saida Mustafa alisema ugawaji wa vyandarua hivyo ni mwendelezo wa hatua, ambazo kampuni hiyo imeshachukua kupambana na ugonjwa wa malaria.
Tanzania ni moja ya nchi zinazofanya vyema katika utekelezaji wa mkakati huo, ikiwa na kampuni zaidi ya 40 zinazoshiriki katika kupambana na malaria kwa wafanyakazi wake, familia zao na jamii.

No comments: