ZANA HARAMU ZA UVUVI ZA MILIONI 68.6/- ZATEKETEZWA

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Rachel  Kassanda ameshiriki katika hafla ya kuteketeza zana haramu za uvuvi zenye thamani ya Sh milioni 68.6. Shughuli hiyo ilifanyika wilayani Muleba mkoani Kagera.
Kabla ya kuteketeza zana hizo alisomewa risala na Ofisa Uvuvi wa wilaya hiyo, Senfolian Ngaza ambaye alisema zana hizo zilizoteketezwa zilikamatwa katika operesheni iliyofanyika ndani ya Ziwa Victoria kati ya Machi na Aprili, mwaka huu.
Ngaiza alizitaja zana hizo kuwa ni nyavu na makokoro yenye macho madogo chini ya sentimeta tano ambazo zilikamatwa na kikosi cha doria na uvuvi cha Muleba.
Alisema pamoja na jitihada za Serikali, wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano katika jambo hilo  la  kukomesha  uvuvi haramu ili kuondokana na hofu, kwamba ifikapo mwaka 2025 samaki aina ya sangara wanaweza kutoweka kabisa katika Ziwa Victoria.
Akichoma zana hizo kiongozi huyo aliwataka wananchi kutunza rasilimali za nchi na mazingira kwa kufanya uvuvi endelevu, kitaalamu na kuvua kwa kufuata sheria za uvuvi, kwani rasilimali hizo zimetolewa na Mungu kwa manufaa ya watu wote na pia wapo waliojitoa nguvu zao na maisha yao katika kuzilinda na kuzienzi zikafikia hapa zilipo hivi sasa .
"Tutunze rasilimali zetu kama mazingira, maziwa na viumbe waliomo kama samaki, tusivue  kwa  zana haramu na sumu, tusivue samaki wachanga, inawezekana wapo wanaofanya hivyo tunawaona tunakataa kuwataja na kutoa taarifa katika vyombo husika kwa kupewa pengine rushwa ya sangara mmoja, tukifanya hivyo tunakuwa hatujitendei haki na hatulitendei haki Taifa letu na vizazi vijavyo kwa hiyo tuwafichue waharibifu, tutunze rasilimali ambapo tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga heshima ya Taifa letu na kuongeza uchumi na kipato chetu na Taifa letu," alisema Kassanda.
Aidha aliwataka vijana kufanya kazi kwa kujituma  na kubuni miradi mbalimbali itakayowaingizia kipato.
Pia Kassanda aliwataka Wanamuleba  kuwa tayari kupiga kura ya maoni ya Katiba mpya muda utakapowadia ambao ni ujumbe wa mwenge mwaka huu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Lembris Kipuyo alisema wilaya hiyo inayo miradi mitano ambayo itazinduliwa na mwenge wa Uhuru. Miradi hiyo imegharimu zaidi ya Sh milioni 305 .9, mwenge wa uhuru unaendelea na mbio zake mkoani Kagera na kesho utakuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.

No comments: