WIZARA YA KILIMO KUDHIBITI SUKARI YA MAGENDO



Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imewaomba wadau wa sekta ya sukari nchini wakiwemo wazalishaji katika  viwanda vya ndani kuendelea kutoa
ushirikiano wa karibu  na  vyombo vya dola kwa kuhakikisha wanawafichua wafanyabiashara wasio waaminifu  wanaoingiza sukari kwa njia ya  magendo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu  Waziri wa Wizara hiyo , Godfrey Zambi,  wakati akizungumza na Menejimeti ya Kiwanda cha Sukari Kilombero , juzi.
Naibu huyo alifanya ziara ya  kuangalia hali ya uzalishaji wa sukari na kupata changamoto kutoka kwa Uongozi wa kiwanda hicho.
Hata hivyo alisema, licha ya viwanda vya ndani  kutokuwa na  uwezo wa kukidhi mahitaji ya sukari nchini, na kuifanya Serikali kulazimika kuziba
 pengo hilo kwa kuagiza sukari toka nje , hatua hiyo isitumike visivyo na wafanyabiashara hao kwa kukiuka utaratibu uliowekwa kisheria.
“ Katika kudhibiti jambo hilo ,TRA imepewa kazi  hiyo
kuona na kuhakikisha sukari inayoingia kwa magendo
inadhibitiwa na pia inayosafirishwa inakuwa chini ya uangalizi maeneo yote” alisema Naibu Waziri.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, TRA pia imepewa jukumu la kupitia upya sheria ya kodi kwa bidhaa hiyo inayoagizwa kutoka nje  ili bei yake isiweze
kuathiri ushindani wa soko  kutoka  viwanda vya hapa nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi  Mkuu wa Kiwanda cha Sukari Kilombero, Joseph Rugaikamu  alitoa taarifa ya hali ya uzalishaji wa sukari  kwenye kiwanda hicho alisema hadi kufikia Mei 17, mwaka huu kilikuwa na  tani   za sukari 24,999 zilizokosa soko.
Naye  Meneja Maendeleo Mipango na Uratibu wa Bodi ya Sukari nchini, Abdul Mwamkemwa ,alisema   katika kudhibiti uingizaji wa sukari na magendo na kutolipiwa kodi , Mamlaka ya Mapato  Tanzania (  TRA ), ndio wenye jukumu la kusimamia   na tayari wamebuni njia mbadala ya kudhibiti hali hiyo ambayo itaondoa hali inayojitokeza kwa sasa.

No comments: