WAZIRI ATAJA CHANGAMOTO ZA NGO KUTEGEMEA WAFADHILI


Idadi ya mashirika yasiyo ya kiserikali imeongezeka kutoka 3,000 mwaka 2001 hadi kufikia 6,427  Machi mwaka huu ambapo kati ya hayo mashirika 254 ni ya kimataifa. 
Hayo yalisemwa jana na Waziri  wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake bungeni. 
Alisema kwa sasa Tanzania ina Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) 6,427, lakini mengi yao ni tegemezi na hivyo kuathiri shughuli za utendaji pindi wafadhili wanapositisha misaada.
“Kuna changamoto zinazohitajika kufanyiwa kazi kwani sehemu kubwa  za NGOs kutegemea wafadhili kutoka nje na hiyo kuathiri uendelevu wa shughuli hizo pindi ufadhili unapokoma,” alisema. 
Pia alisema kutokuwepo kwa kamati za maadili ya NGOs katika baadhi ya Mikoa na Wilaya  kunakoathiri uwezo wa mashirika hayo kujitawala katika kuongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali na uendeshaji wa mashirika hayo. 
Alisema katika kukabiliana na changamoto hizo serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuhimiza mashirika yasiyo ya kiserikali kutumia fursa ya marekebisho ya sheria ya NGOs yaliyofanyika mwaka 2005 kuanzisha na kuendeleza miradi ya kuzalisha faida kwa ajili ya kutekeleza malengo pale wafadhili wanapositisha misaada. 
Pia Wizara kupitia Baraza la Taifa la NGOs kuliwezesha kuanzisha kamati za maadili ya NGOs  katika ngazi za wilaya za mikoa, ikiwa ni utekelezaji wa kanuni za maadili na NGOs.
Akizungumzia ukatili dhidi ya watoto, alisema wizara iliendelea kuratibu  utoaji wa taarifa za ukatili  dhidi ya watoto kupitia namba ya simu 116 inayosimamiwa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la C-SEMA. 
Alisema hadi kufikia  Machi 2014 jumla ya simu 6,188  zilipigwa kutumia namba hiyo na kufanyiwa kazi mbapo katika mwaka 2014/2015 wizara itaendelea kutathmini ili kuwezesha  kupeleka huduma katika maeneo mengi ya nchi. 
Pia alisema ushiriki wa  wanawake katika ngazi za siasa na maamuzi iliongezeka ambapo Mawaziri wanawake waliongezeka kutoka asilimia 15 mwaka 2005 hadi asilimia 30 mwaka 2013, wakuu wa mikoa wanawake kutoka asilimia 10 mwaka 2005 hadi asilimia 24 mwaka 2013. 
Hata majaji wanawake pia wameongezeka kutoka asilimia 33 hadi 61 kwa kipindi hicho na uwakilishi wa wanawake bungeni umeongezeka kutoka asilimia 3.3 mwaka 2005 na kufikia asilimia 36 ya wabunge wote mwaka 2013. 
Akichangia katika hotuba hiyo Mbunge wa Viti Maalumu, Getrude Rwakatare (CCM)  alitaka kukemewa kwa ukatili wa kingono ikiwemo ndoa za jinsia moja. 
“Kumpiga mwanamke ni aibu na ushamba, mwanamke anapigwa na khanga,  kitenge, mwanamke anapigwa na mkufu wa dhahabu, mke  sio ngumi, mke wako, mama, watoto wako unampiga kwa nini, wakati kuna wazee na hata wachungaji wanaoweza kuwasaidia mkaelewana,” alisema. 
Alisema  mke na mume wanatakiwa kupendana na kushikamana siku zote za maisha yao. 
Waziri Simba aliomba Bunge kuidhinisha matumizi ya Sh bilioni 30.2  kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo.

No comments: