Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameomba kuwepo na maridhiano ya madai
ya `waumini’ wa kinachoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili warejee
katika Bunge la Katiba ili kukamilisha kazi ya kutengeneza Katiba mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa wazee hao, Erasto Singila alisema pamoja na
wao kuunga mkono hatua ya Ukawa kutoka bungeni, lakini wanaona ni vyema madai
yao, yakasikilizwa ili kuwepo na maridhiano.
“Tunaunga hatua ya Ukawa kutoka, kwa
kile tulichokuwa tukiona kikiendelea ndani ya ukumbi wa Bunge, lakini Katiba
mpya tunaitaka, ila madai yao
yasikilizwe kuwe na maridhiano ili warejee”, alisema Singila.
Alisema kwa mwenendo wa sasa, ni vigumu
Katiba mpya kupatikana na kwamba hata ikipatikana, itakuwa sio yenye maridhiano
ya pande zote, wala sio ya wananchi, bali itakuwa imeegemea upande mmoja, hivyo
ni vyema maridhiano yakapewa nafasi.
Katika hatua nyingine, Singila alisema
leo wameandaa kongamano la wazee, linalofanyika katika ukumbi wa Kituo cha
Msimbazi jijini Dar es Salaam, lenye lengo la kuwakutanisha wazee wa maeneo tofauti ya Kanda ya
Pwani wa chama hicho, kujadili masuala
mbalimbali.
Kongamano hilo, litakalofunguliwa na
Profesa Abdallah Safari, litazungumzia mada nne, ikiwemo suala la Ukawa na
yaliyojiri bungeni, Ushiriki wa wazee katika Chama, huduma za wazee na
maendeleo na rasilimali za nchi.
Singila aliongeza kongamano hilo, pia
litazungumza kwa urefu juu na mtazamo kuhusu wazee na kwamba sio kweli kuwa
wazee ni waoga, bali wapo imara kuangalia mambo yanayojiri nchini.
Alisema katika mada hizo, suala la
wazee litapewa kipaumbele, ambapo watazungumza mambo wanayotaka yawepo, ikiwemo
sera bora kuhusu wazee, kwani wamelitumikia taifa kwa muda mrefu na sasa
wanapaswa kuthaminiwa na kutunzwa.
No comments:
Post a Comment