WAWEKEZAJI WA MRADI WA MABASI YA HARAKA KUKUTANA



Rais Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuongoza mkutano wa mashauriano ya uwekezaji wa awamu ya kwanza ya Mradi wa Mabasi ya Haraka (DART),  utakaowakutanisha wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje kwenye kituo cha mikutano Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa DART, Asteria Mlambo aliwaambia waandishi hivi karibuni kuwa mkutano huo wa mashaurino, utakaofanyika kati ya Juni 3 na 4, mwaka huu, utatoa nafasi kwa wawekezaji kuzijua fursa mbalimbali za uwekezaji zitakazopatika kwenye mradi huo unaojengwa kwa mabilioni ya fedha.
“Washiriki wote kwenye mkutano wa majadiliano, watapata fursa ya kutembelea eneo la mradi na watapata nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wake kuhusu mradi,” alisema Mlambo na kuongeza kuwa mkutano huo ni muhimu.
Akifafanua zaidi, Mtendaji huyo Mkuu alisema benki na taasisi mbalimbali za kifedha, kampuni za kutengeneza mabasi,  kampuni za mawasiliano, mifuko ya kijamii na nyinginezo nyingi zimealikwa kwenye mkutano huo.
 “Mada mbalimbali kuhusu mradi zitatolewa ambapo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini atawasilisha mada kuhusu mradi wa DART,” alisisitiza.
Mlambo alisema kabla ya mkutano huo wa mashauriano mwezi ujao, Wakala ameandaa mkutano utakaowakutanisha wamiliki wote wa daladala jijini Dar es Salaam pamoja na Kampuni ya Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) na wadau wengine, ili kuwafahamisha kuhusu mkutano na kushauriana na ni jinsi gani watanufaika na mfumo.
 “Tutawaelezea faida na fursa zitakazopatikana kwenye mfumo mpya wa usafirishaji jijini na jinsi watakavyokuwa sehemu ya mradi,” alisema Mtendaji Mkuu huyo, na kuongeza kuwa taarifa na ratiba za mkutano zinapatikana kwenye tovuti ya wakala www.dart.go.tz.
Mwezi uliopita, DART ilikamilisha usajili wa mabasi ya daladala yanayopita katika barabara ya Morogoro au kukatiza katika njia hiyo.  
Hatua hiyo ya kuandikisha mabasi hayo ilikuwa moja ya matayarisho ya kupisha mradi huo wa mabasi yaendayo haraka. 
Kwa sasa wakala huo uko kwenye mchakato wa kuwezesha upatikanaji wa watoa huduma kwenye mfumo mpya wa mabasi yaendayo haraka awamu ya kwanza ambayo inajumuisha barabara ya Morogoro, Kawawa na mtaa wa Msimbazi kwa njia kuu na nyingine za kiungo.  
Kulingana na mpango wa uendeshaji wa mfumo wa DART, barabara zinazohusika, zitapaswa kutumiwa na mabasi ya mfumo huo pekee.
Jumla ya ruti  64 jijini Dar es Salaam, zitakoma kutumika kutokana na kuanza kwa mradi huo.

No comments: