WATUMIAJI BARABARA YA DAR-CHALINZE KUANZA KULIPIAWizara ya Ujenzi imesema inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa barabara mbadala kati ya Dar es Salaam na Chalinze kwa kiwango cha Expressway na itakuwa ya kulipia yenye njia sita.
Waziri Dk John Magufuli alibainisha hayo juzi usiku wakati alipowasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2014/15. Aliliomba Bunge liidhinishe bajeti ya Sh 1,219,717,592,000.
Dk Magufuli alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 100, itajengwa kwa utaratibu wa kushirikisha Serikali na Sekta Binafsi (PPP).
“Barabara hiyo mbadala ambayo itakuwa ni ya kulipia, itajengwa kwa njia sita (6 lanes). Barabara iliyopo sasa itaendelea kutoa huduma kwa wale ambao hawako tayari kutumia barabara ya kulipia,” alisema Dk Magufuli na kuongeza:
“Wizara imefanya maandalizi ya ujenzi wa mradi huu ikiwa ni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu wa awali (pre-feasibility study), kutoa tangazo la kualika kampuni kuonesha nia (Expression of Interest) ya kushiriki katika ujenzi wa barabara hii kwa utaratibu wa PPP ambapo kampuni 12 zimeonesha kuwa na uwezo wa kujenga barabara hiyo.”
Alisema Wizara inaendelea na taratibu za kumpata Mtaalamu Mwelekezi wa mradi ambaye ataisaidia Serikali katika kufanya upembuzi yakinifu na usanifu, kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya kumpata mbia pamoja na kushauri masuala ya kifedha na kisheria.
Akizungumzia Barabara ya Nelson Mandela, alisema mwaka ujao wa fedha imetengewa Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya kulipa malipo ya mwisho ya mkandarasi, kwa ajili ya kuimarisha njia hiyo ili kurahisisha usafiri wa magari ya mizigo yanayotoka Bandari ya Dar es Salaam, hivyo kupunguza msongamano jijini.
Aidha, alisema katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, maandalizi ya upanuzi wa Barabara ya Nelson Mandela sehemu ya Dar Port – Tazara ya kilometa sita, yataanza katika mwaka 2014/15 kwa njia sita. Zimetengwa Sh bilioni 150 kwa ajili ya maandalizi ya upanuzi kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Kuhusu njia za juu “flyovers”, Dk Magufuli alisema Sh bilioni moja za ndani na Sh bilioni 15 fedha za nje, zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa “flyover” ya Tazara.
Aidha, alisema zimetengwa Sh milioni 100 kwa ajili ya kulipa fidia kwa mali na kuhamisha miundombinu ya huduma za kijamii zitakazoathirika na ujenzi wa “flyover” hiyo eneo la Tazara.
Kuhusu ukarabati na kupanua barabara ya lami ya sehemu ya Gerezani (Kamata – Bendera Tatu) kutoka njia mbili za sasa hadi njia nne chini ya msaada kutoka Serikali ya Japan na Serikali ya Tanzania, usanifu wa kina na utayarishaji wa zabuni umekamilika.
“Kazi ya kuhamisha miundombinu iliyoko eneo la ujenzi zinaendelea. Aidha, taratibu za kutafuta mkandarasi zinaendelea. Katika mwaka wa fedha 2014/15, mradi huu umetengewa Sh milioni 2,000 fedha za ndani na Sh milioni 6,000 fedha za nje kwa ajili ya kukamilisha ulipaji fidia na kuanza ujenzi wa sehemu ya Kamata – Bendera Tatu (kilometa 1.5),” alisema Dk Magufuli.

No comments: