WATOTO TANZANIA KUSAIDIA UTENGENEZAJI KINGA YA MALARIAKundi la watoto nchini Tanzania wenye kinga asilia ya malaria, wanawasaidia wanasayansi kutengeneza kinga mpya ya ugonjwa huo.
Watafiti wa Marekani wamebaini miili ya watoto hao, hutoa viini vya kinga ambavyo hushambulia wadudu wanaosababisha malaria.
Watafiti hao walisema mtu akidungwa sindano yenye viini hivyo vya kinga asilia vya binadamu, vinaweza kumkinga na ugonjwa huo.
Ripoti ya watafiti hao imechapishwa katika  jarida la kisayansi nchini humo, na kusema majaribio ya utafiti huo, yalifanywa kwa sokwe na binadamu na kwamba hivi sasa yanahitaji kutathminiwa kikamilifu ili kupata matumaini halisi ya chanjo ya malaria.
Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Afya cha Kimataifa katika Hospitali ya Kisiwa cha Rhode cha Chuo Kikuu cha Tiba cha Brown, Profesa  Jake Kurtis, alisema anaamini upo ushindi wa kuaminika na matokeo hayo ni ishara ya upatikanaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa huo.
"Hata hivyo wadudu wa malaria ni vigumu kuwashambulia, ni maadui wakubwa wa fya ya binadamu", alisema Kurtis.
 Utafiti huo ulianza kwa kundi la watoto  1,000 nchini Tanzania, ambao sampuli za damu yao zilichunguzwa mara kwa mara katika miaka ya mwanzo ya maisha yao .
Kati ya sampuli hizo, asilimia sita ya watoto hao waliochukuliwa sampuli walikuwa na kinga asilia dhidi ya malaria, licha ya wao kuishi katika eneo ambalo ugonjwa huo umekithiri.
Taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2012, zinasema ugonjwa wa malaria umeua watu zaidi ya 600,000, huku asilimia 90 ya vifo hivyo ni vya wagonjwa kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara,  ikiwemo Tanzania.

No comments: