WATANZANIA WAHIMIZWA KUOMBA VITALU VYA MIFUGO



Serikali imewataka Watanzania kuwa mashujaa wa kuomba vitalu vya uwekezaji katika mashamba ya mifugo vinapotangazwa badala ya kuwaachia watu kutoka nje.
Aidha, Wizara ya Fedha imesema itatoa Sh bilioni 10.5 kati ya takribani Sh bilioni 20 zilizosalia ambazo zilitengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14 ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, ili kukamilisha baadhi ya miradi ya maendeleo.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani alisema hayo juzi jioni wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2014/15 bungeni mjini hapa.
Dk Kamani alisema: “Watanzania tuwe mashujaa katika kuomba vitalu vya uwekezaji. Watanzania wengi wanaogopa. Vitalu hivi si kwa ajili ya watu wa nje pekee. Ni muhimu kuwatambua wazawa.”
Waziri alisema hadi sasa kuna vitalu 105 vya mashamba ya uwekezaji ambavyo vimebinafsishwa kwa wawekezaji, na kurejea kauli yake kwamba vile ambavyo havifanyi vizuri, Serikali itavichukua na kuvigawa upya.
Akizungumzia ruzuku kwa wavuvi, alisema katika mwaka ujao wa fedha zimetengwa Sh bilioni 2.2 kwa ajili ya wavuvi wadogo, tofauti na madai ya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), kwamba hakukuwa na fedha hizo katika bajeti ya waziri.
Aidha, alikubaliana na michango ya wabunge wengi kuwa sekta ya mifugo na uvuvi, ikitumiwa fedha, itasaidia sana kuleta tija na ufanisi na kukuza uchumi wa Taifa.
Kuhusu fedha za bajeti inayomalizika, Waziri huyo pamoja na Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, walitangaza kwamba Hazina itatoa Sh bilioni 10.5 ili zikamilishe baadhi ya miradi iliyopangwa kufanyika katika mwaka huo wa fedha unaoishia Juni 30, 2014.
Wakati Bunge lilipokaa kama Kamati kupitisha bajeti hiyo, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), alizungumzia suala la migogoro ya wafugaji na wakulima na kutaka kufahamu hatua ambazo waziri huyo  pamoja na Naibu wake, Kaika Telele ni wapya katika wizara, watachukua kukomesha kadhia hiyo.
Hoja yake iliibua mjadala mkali, lakini mwishoni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema Kamati iliyoundwa na Bunge chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji, Profesa Peter Msolla imekamilisha kazi yake na ripoti iko kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu aliyekuwa akiendesha kikao cha juzi, alilieleza Bunge kuwa atamshauri Spika kuiwasilisha haraka bungeni ripoti hiyo ili ijadiliwe; hoja ambayo ilikubaliwa na Msigwa ambaye alitangaza kuondoa Shilingi katika mshahara wa Waziri.

No comments: