WATANZANIA WAHIMIZWA KUNYWA MAZIWA

Bodi ya Maziwa nchini kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la Heifer International, wameanzisha mpango maalumu wa kuhamasisha unywaji wa maziwa nchini ili kuwezesha watu wengi zaidi wakiwemo watoto kuwa na mwamko wa unywaji wa maziwa.
Katika kuhakikisha mpango huo maalumu  unafanikiwa, shirika hilo lisilokuwa la kiserikali limetoa kiasi cha Sh milioni 30  kwa ajili ya kuwezesha bodi hiyo kufanya maonesho ya kitaifa kuhusu sekta ya maziwa na usindikaji bidhaa zake pamoja na Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Wadau wa Maziwa nchini.
Maonesho hayo ya Wiki ya Maziwa yakiwa na kauli mbiu Fuga ng’ombe wa maziwa uboreshe kipato na lishe “badilika sasa” yanafanyika kitaifa katika Mji wa Musoma mkoani Mara kuanzia jana hadi June mosi mwaka huu katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Mkendo.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Dk Henry Njakoi, amesema pamoja na Tanzania kuwa nchi ya tatu kwa kuwa na ng'ombe wengi lakini ndio nchi ya mwisho kwa nchi za Afrika Mashariki katika unywaji wa maziwa.
Tanzania sasa inakadiriwa kuwa na ng’ombe milioni 22, ikiwa ni nchi ya tatu Afrika kuwa na ng'ombe wengi. Tanzania inatanguliwa na Ethiopia na Sudan.

No comments: