WATANO MBARONI KWA TUHUMA ZA KUVUNJA MSIKITI


Watu watano  wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Ilala, kujibu mashitaka ya kuvunja msikiti. 
Watu hao ni Mohamed Ngwai (31), Issa Karim(40), David Kambarage (32), Melkiori Utoh (33)na Athuman Msagati (30).Wakili wa Serikali,  Ester Kyala alidai mbele ya Hakimu John Msafiri kuwa Mei 2 mwaka huu eneo la Zanaki Wilaya ya Ilala, washitakiwa hao walivunja  msikiti wa Satan Zamra. 
Washitakiwa walikana mashitaka. Kati ya hao, Ngwai na Utoh waliachiwa huru baada ya kutimiza masharti ya dhamana. 
Hakimu Msafiri aliwataka kuwa na wadhamini wawili wa kuaminiwa, watakaosaini kulipa  Sh milioni moja. 
Wakati huo huo, mkazi wa Mwananyamala Kisiwani amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Ilala, kujibu mashitaka ya wizi wa kutumia silaha.
Wakili wa Serikali, Hilda Kato alidai mbele ya Hakimu, Alfred Sachore  kuwa Oktoba 13 mwaka 2011 maeneo ya Kinyerezi  Wilaya ya Ilala, mshitakiwa aliiba Sh milioni 1.7, dola za Marekani 400.
Vitu vingine ni simu ya mkononi aina ya Samsung yenye thamani ya Sh 400,000, kompyuta ndogo ya Sh 1,600,000, vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 5.2, mali ya Angumwike Lameck.
Kabla ya tukio hilo, mshitakiwa alitumia kitu chenye ncha kali, kumtishia Lameck ili kufanikisha wizi. Mshitakiwa alikana mashitaka hayo na yaliahirishwa hadi Mei 30 mwaka huu watakapoanza kusikiliza ushahidi.

No comments: