WATAKAOHAMISHWA MAKAMBAKO KULIPWA SHILINGI BILIONI 1.2

Wananchi 217 wanahamishwa katika eneo la Mji Mwema lenye ekari 62 kwa ajili ya ujenzi wa  wa soko la kimataifa la Makambako.
Tathimini ya awali ilionyesha kuwa watu hao wanatakiwa kulipwa fidia ya Sh bilioni 2.175.
Ili kufanikisha malipo ya fidia kwa wananchi watakaopisha ujenzi huo, Halmashauri ya Mji wa Makambako imekubaliana na Benki ya Uwekezaji ya TIB, kulipa fidia hiyo ili kuharakisha ujenzi wa soko hilo.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene alisema hayo jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Njombe Kaskazini, Deo Sanga (CCM) aliyetaka kujua soko hilo litajengwa lini  na wananchi hao watalipwa fidia lini.
Akijibu swali hilo, Mbene alisema wizara kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Njombe  na Halmashauri ya Mji wa Makambako, imekamilisha upembuzi yakinifu na kutenga eneo la sokolenye ekari 62.
Pia, kuandaa mpango kabambe wa utekelezaji, tathmini ya athari ya mazingira imefanya inasubiriwa hati na michoro imeishakamilika na kuwasilishwa Wizara ya Ardhi kwa ajili ya kupatiwa hati miliki.
Alisema pia wizara imefanya mazungumzo na Benki ya TIB, kuhusu upatikanaji wa rasilimali za ujenzi wa soko na mwanzoni mwa mwaka huu wametembelea eneo hilo na kufanya mazungumzo na rasimu ya makubaliano iliwasilishwa kwa ofisi ya Mkurugenzi na inasubiriwa ili kukamilisha taratibu za utiaji saini.
“Nichukue fursa hii, kuomba mkurugenzi wa Halmashauri ya Makambako kuridhia  na kuipitisha rasimu hiyo haraka na kuiwasilisha TIB kwa ajili ya hatua zaidi kwani benki hiyo wameshindwa kuendelea na taratibu nyingine wakisubiri ukamilishwaji huo,” alisema.
Mbene alisema fedha zitakazolipa fidia, zitatoka TIB na  zitakuwa sehemu ya gharama za mradi. Baada ya kukamilika, taratibu za malipo fidia zitalipwa pamoja na malimbikizo yake kwa walengwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999, ambayo ndiyo inayotumika sasa.

No comments: