WASICHANA 1,498 WAPEWA MAFUNZO YA UFUNDIChuo cha Ufundi Arusha kimefanikiwa kuwajengea uwezo wa kujiamini wasichana zaidi ya 1,498 kwa kuwapatia programu mbalimbali za ufundi.
Wamepewa mafunzo hayo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wasichana wengi wanaingia katika soko la ajira.
Katika mafunzo hayo, wamejengewa uwezo katika fani za uhandisi ufundi, uhandisi umwagiliaji, ufundi magari, ufundi umeme na programu nyingine zinazoendeshwa na chuo hicho.
Hayo yameelezwa  na Mhadhiri Msaidizi katika Idara ya Umwagiliaji chuoni hapo, Dk Nuru Mziray.
Alisema chuo kinahakikisha wanafunzi wa kike kuanzia msingi na sekondari, wanahamasishwa kusoma masomo ya sayansi kuanzia mwanzo.
Pia alisema chuo hicho kimekuwa kikiwafuatilia maendeleo yao mpaka wanapomaliza elimu ya msingi ama sekondari na kuwasisitizia umuhimu wa masomo ya sayansi na teknolojia kwao.
Mziray alisema Tanzania idadi ya wasichana wanaoamua kusoma masomo ya sayansi wakiwa katika shule za sekondari na vyuoni ni ndogo mno.
Alisema katika mwaka ujao wa masomo, chuo kimepanga kuchukua wasichana 411 wa fani mbalimbali.

No comments: