Katika kuhakikisha kunakuwa na uhifadhi endelevu wa wanyamapori nchini, serikali imetangaza kuanzisha Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori inayotarajiwa kuanza kazi mwishoni mwa mwezi huu huku makao yake makuu yakiwa mkoani Morogoro.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema
sambamba na uanzishwaji wa mamlaka hiyo, pia itaundwa bodi maalumu itakayokuwa
na wajumbe wasomi na waadilifu ambao wataleta ushindani katika sekta hiyo
umuhimu.
Nyalandu alisema hayo jana wakati akihutubia Mkutano
wa Kimataifa wa Kuzuia Uhalifu wa Wanyamapori na kuendeleza Uhifadhi wa Wanyamapori
uliokutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, jumuiya za
kimataifa, wafanyabiashara na wadau wengine katika sekta ya utalii na
maliasili.
Aidha, Nyalandu alisema pia wanatarajia kuanzisha Bodi
ya Nidhamu itakayosimamia kanuni za maadili wakati askari wanyamapori
wakitekeleza majukumu yao ili kudhibiti yasitokee kama yale yaliyotokea wakati
wa Operesheni Tokomeza.
Nyalandu alisema matarajio ya mkutano huo wa siku
mbili ni serikali kujadili na wadau mbalimbali kuona njia bora zaidi ya
kukabiliana na ujangili na kulinda tembo wa Tanzania.
Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal akifungua
mkutano huo alisema Sekta ya Maliasili na Utalii imekuwa ikichangia kwa kiasi
kikubwa Pato la Taifa pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni
pamoja na ujangili, ongezeko la uhitaji wa bidhaa za wanyamapori na uharibifu
unaofanywa na wakazi.
Aidha Dk Bilal alisema ukosefu wa fedha za kutosha,
vifaa, teknolojia na mafunzo ni changamoto kubwa na kuitaka Jumuiya ya
Kimataifa kusaidia katika maeneo hayo ili askari hao waweze kukabilianana
wahalifu hao.
“Tafadhali Jumuiya ya Kimataifa na marafiki tunaomba
mtuunge mkono na kutusaidia kuchukua hatua za kiusalama kuhakikisha tunalinda
tembo wetu wasiendelee kuteketezwa na majangili,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Kimataifa inayosimamia
Hifadhi (ICCF-Group), Dk Kaush Arha alisema Urithi wa Asili umevamiwa na kwamba
wadau wamekutana pamoja kujadiliana na kutoka na hatua maalumu na namna ya
kuziendeleza au kuziboresha.
No comments:
Post a Comment