WANAVIJIJI WAVAMIA RANCHI YA KONGWA



Ranchi ya Taifa  ya Kongwa (Narco) iliyoko wilayani Kongwa mkoani Dodoma, imevamiwa na wanavijiji ambao wamefanya uharibifu mkubwa katika eneo la hifadhi yake. 
Pamoja na uharibifu wa hifadhi yake, wananchi hao wamekuwa wakiiba na kuua baadhi ya mifugo na kujeruhi. 
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Ranchi ya Taifa Mwandamizi Heslon Kashalankolo wakati akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki waliotembelea hifadhi hiyo. 
Meneja huyo alisema ranchi hiyo imeharibiwa kwa asilimia 70 kutokana na wananchi kuvamia na kulima mashamba makubwa yakiwemo ya mahindi ndani ya hifadhi. 
Aliongeza kuwa hata maisha ya wafanyakazi wa ranchi hiyo yako mashakani kutokana na wengi wao kuvamiwa na wananchi hao wakiwa machungani na kuporwa ng’ombe huku baadhi yao wakiuawa na kufukiwa na wananchi hao ili kupoteza ushahidi. 
Alisema mwaka jana kuna mfanyakazi wao mmoja aliuawa akiwa machungani na kumzika porini, ambapo baada ya kutomwona kwa siku tatu waliamua kumtafuta na ndipo walipokuta kaburi lake porini.  
“Kwa kipindi cha kuanzia  mwaka 2010 hadi mwaka 2013, ranchi imepoteza wafanyakazi wake watatu kwa kuuawa na wananchi wakiwa machungani na wengine 16 wamejeruhiwa kwenye majaribio mbalimbali ya wizi wa ng’ombe,” alisema Kashalankolo. 
Kwa upande wake mbunge wa Longido, Michael Laizer, alipotembelea ranchi hiyo na kujionea uharibifu mkubwa wa mazingira uliofanyika aliitaka Serikali  kuumaliza mgogoro huo kwani upo ndani ya uwezo wake. 
Ranchi hiyo ya Taifa ilianzishwa mwaka 1948 ambapo ina ukubwa wa hekta 38,000 na mifugo 8,000 wakiwemo ng’ombe, farasi, mbuzi na kondoo ambao hufugwa kisasa.

No comments: