WANAOJIDUNGA DAWA ZA KULEVYA WANA VIRUSI VYA UKIMWI



Asilimia 36 ya watu wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano nchini, wana maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Takwimu hizo huenda  zikaongezeka, ikiwa jamii haitaelimishwa jinsi ya kupunguza madhara dhidi ya dawa hizo.
Hayo yalisemwa  jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Mtandao wa Watu wanaotumia Dawa za kulevya (TanNPUD), Happy Assen kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Madhara kwa watumia dawa za kulevya.
Alisema ingawa matumizi ya dawa za kulevya ni makubwa nchini, bado jamii haiko karibu na watu wanaotumia dawa hizo, na badala wametengwa kama wahalifu, na kusahau kwamba nao pia ni sehemu ya jamii na wanapaswa kusaidiwa.
“Wanajamii wana mtazamo hasi kuhusu upunguzaji madhara kwa watumia dawa za kulevya, wengi wanadhani upunguzaji madhara unachangia ongezeko la matumizi ya dawa hizo kwenye soko, jambo ambalo sio sahihi,” alisema Assen.
Alisema takwimu za afya na matumizi ya dawa za kulevya nchini, zinaonesha asilimia 36 ya watumia dawa za kulevya nchini kwa njia ya kujidunga sindano, wamepata maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Alisema hiyo inatokana na watumia dawa hizo, kuchangia bomba moja la sindano watu wengi wakati wa kujidunga dawa za kulevya aina ya heroine, kwa sababu hawana uwezo wa kumudu gharama za kununua kila mmoja bomba lake.
Takwimu za hivi karibuni nchini  za matumizi ya dawa za kulevya, zinaonesha kwamba watu wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano ni 25,000, na kati ya hao 18,000 wapo Dar es Salaam.
Alisema, TaNPUD kwa kushirikiana na wataalamu wa masuala ya Video na Afya ya Maendeleo(VAMA), wameandaa  onesho litakalofanyika jijini Dar es Salaam  kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu upunguzaji madhara kwa watumia dawa za kulevya, ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

No comments: