WANAJESHI WAMTUMIA SALAMU RAIS KIKWETEWanajeshi nchini, wamemwahidi Rais Jakaya Kikwete kuendelea kusimama imara, kupokea na kutii amri na maelekezo yake bila hila na kuhakikisha
hawayumbishwi na kauli potovu za kisiasa.  
Ahadi hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi kwa niaba ya wanajeshi wakati akiwasilisha makadirio ya  bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2014/15. 
Dk Mwinyi ambaye wizara yake iliomba kuidhinishwiwa Sh trilioni 1.3, aliwasilisha shukurani za wanajeshi kwa Rais Kikwete, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu kwa hiba yake ya uongozi, ushupavu, uvumilivu na maridhiano vitakumbukwa na kuenziwa na vizazi na vizazi hususani kwao. 
 “Ahadi yetu kwake ni kuwa tutaendelea kusimama imara kupokea na kutii amri na maelekezo yake bila hila yoyote na kutoyumbishwa na kauli potovu za kisiasa,” alisema Dk Mwinyi na kushangiliwa bungeni. 
Aidha katika hotuba hiyo ya Waziri, aliwasilisha salamu za pongezi za Rais Kikwete kwa wanajeshi wote kwa kufanikisha maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanzania. 
Katika salamu hizo, Rais Kikwete alisema kazi iliyofanywa na wanajeshi ni kubwa na waliifanikisha kwa weledi, utii, uhodari, ujasiri na kwa kishindo cha hali ya juu. 
 “Ushiriki wao umedhihirisha umma wa Watanzania na ulimwengu kwa ujumla kuwa jeshi letu ni imara, shupavu na lipo tayari kulinda, kutetea na kudumisha Muungano wetu…nami nikiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa natamka kuwa najivunia nao,” alisema Dk Mwinyi. 
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, katika taarifa yake iliyosomwa na Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa, pia imepongeza wizara na vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri ya ulinzi na usalama wa nchi na hivyo kudumisha amani, utulivu na umoja wa nchi. 
Pia ilipongeza majeshi  yote kwa kufanikisha sherehe za Muungano ambazo kwa mujibu wa kamati, zilifana na kuhakikishia Watanzania kuwa nchi iko salama. 
Awali, akizungumzia bajeti ya wizara yake, Dk Mwinyi alitaja changamoto za utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2013/14, alisema kulikuwa na changamoto kubwa katika utekelezaji wake kutokana na kuidhinishiwa kiwango kidogo cha Bajeti ikilinganishwa na mahitaji halisi. 
Alitoa mfano katika mwaka huo wa fedha, wakati mahitaji halisi kwa kuzingatia vipaumbele vya wizara yalikuwa ni Sh trilioni 1.74, bajeti iliyoidhinishwa ilikuwa Sh trilioni 1.1 sawa na asilimia 63.3 ya mahitaji. 
Kamati ilizungumzia pia ufinyu wa bajeti na kushauri
Serikali kutoa kwa wakati fedha zote zinazoidhinishwa na Bunge kila mwaka.
Wakichangia kwa nyakati tofauti, wabunge wengi walitetea wanajeshi na kutaka Serikali iendelee kuwajali wawapo kazini na wanapostaafu. 
Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM) alisema ni lazima jeshi liwezeshwe hususani vikosi vinavyotengeneza zana, Serikali ihakikishe inanunua vifaa hivyo badala ya kununua nje ya nchi. 
 “Wakati wa amani ndiyo wakati wa kutoa jasho jingi, ukitoa jasho wakati huu, ikija kutokezea damu itakuwa kidogo sana…Umoja wa Mataifa unapenda majeshi yetu,” alisema. 
Kwa upande wake Mbunge wa Chambani,  Yussuf Salim Hussein (CUF)m alitaka stahiki za wanajeshi ziangaliwe upya na kusema haipendezi kukuta mwanajeshi mstaafu akiwa katika hali mbaya. 
Mbunge wa Manyoni, John Chiligati (CCM) alisema amani na utulivu vinavyoonekana, vinatokana na kuwepo Watanzania ambao usiku na mchana wanailinda nchi. 
Alisema kulinda amani ni aghali hivyo Serikali lazima iwekeze kwenye vyombo vya ulinzi na usalama. Alitaka vyombo hivyo visichukuliwe kama vyombo vya kawaida. 
Chiligati ambaye ni mwanajeshi mstaafu, alisema wastaafu mambo yao hayajakaa vizuri. Alisema kamati ilitembelea Bunge la India ambalo miongoni mwa mambo waliyotaka kujifunza ilikuwa ni namna wanavyohuduma
wanajeshi wastaafu. Chiligati alishauri  askari hao waendelee kuundiwa mfumo wa kijeshi wawapo uraiani baada ya kustaafu. 
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid  (CUF) ameshauri viongozi kuwa makini katika matamshi yao kuepuka kuchochea uvunjifu wa amani.
Alisema jeshi  linafanya kazi nzuri na kusisitiza kuwa watu wanaodhani vita ni kitu cha kawaida, wafuatilie nchi zilizokumbwa na machafuko. 

No comments: