WANAHISA CRDB WASHAURIWA KUTOUZA HISA ZAO





Wanahisa wa benki CRDB, wameaswa kuacha kuuza hisa zao badala yake waendelee kuziweka na kujengewa uwezo, ili wapate maendeleo zaidi.
Aidha benki hiyo inatarajia kuanza kuuza hisa zake nchini Kenya, ili kuiwezesha kupata manufaa zaidi pamoja na kuboresha masuala mbalimbali yanayohusu benki.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Dk Charles Kimei, alisema hayo wakati alipozungumza  na  waandishi wa habari kuhusu Mkutano Mkuu wa 19 unaotarajia kuanza jijini hapa leo, uliotanguliwa na mkutano wa awali ulioshirikisha wanahisa wa benki hiyo pamoja wanachama.
Alisema ni vyema wanahisa wawe na tabia ya kuendelea kuwa na hisa zao na kupata elimu juu ya faida za hisa walizonazo katika kuboresha masuala mbalimbali ya kimaendeleo badala ya kuziuza kwa watu wengine kwa bei ya juu.
Alisema pia benki hiyo inatarajia kuanza kuuza hisa zake nchini Kenya kwenye soko la hisa lengo ni kuhakikisha wanashindana katika kupata maendeleo kupitia hisa za benki hiyo.
Alisema mkutano huo wa mwaka pia utapitia ripoti ya Bodi ya Wakurugenzi itakayotoa maendeleo ya utekelezaji wa sera za benki pamoja na kutoa ripoti ya hesabu za mwaka 2013 zilizokaguliwa na mkaguzi wa nje.

No comments: