WALIMU WA SAYANSI NA HISABATI SASA WAULA



Serikali inatarajia kuweka utaratibu maalumu wa ajira kwa walimu wenye ufaulu wa juu katika elimu ya sekondari, watakaojiunga kusomea Stashahada ya Ualimu wa Sayansi na Hisabati chini ya utaratibu wa kupewa ruzuku na mikopo.  
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2014/2015 aliyosoma bungeni mjini hapa.  
Dk Kawambwa  alisisitiza azma ya Serikali kuimarisha vigezo na utaratibu wa kupata walimu wa elimu ya msingi na sekondari kwa kutumia kigezo cha ufaulu wa daraja la tatu katika elimu ya sekondari. Alisema hiyo ndiyo sifa ya chini ya kujiunga na kozi ya ualimu katika ngazi yoyote ya ualimu. 
Alisema  katika kuhakikisha elimu bora inatolewa, wameweka utaratibu wa kuanza kutoa ruzuku na mikopo kwa wanachuo wenye sifa watakaojiunga na mafunzo ya Stashahada ya Ualimu wa Sayansi na Hisabati ili kuvutia wenye ufaulu wa juu na wenye sifa linganishi, kujiunga na ualimu katika maeneo hayo.  
Alisema Wizara kwa kushirikiana na  Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, itaweka utaratibu maalumu kuhusu ajira ya walimu watakaopatikana kupitia utaratibu huo ili watumishi hao  watumikie jamii kama inavyotarajiwa.  
Alisema wamerejesha utaratibu wa kujiunga na mafunzo ya ualimu kwa walimu wa sekondari kwa masomo ya sayansi kwa miaka mitatu kwa wahitimu wa kidato cha nne. Utaratibu huu unaanza kutekelezwa rasmi Julai mwaka huu.  
Hata hivyo, Waziri Kawambwa alisema pamoja na mikakati mbalimbali kufanyika, bado mwendo ni mrefu wa kufikia lengo la kumwandaa mwalimu mahiri na mwenye weledi wa kutosha.  
“Hili linahitaji wadau wote tuendelee kushirikiana…wizara yangu itaendelea kutimiza wajibu wake katika upatikanaji wa walimu bora nchini,” alisema Kawambwa.  
Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri Kawambwa, kwa sasa taifa lina upungufu wa walimu 30,949 wa shule ya msingi na walimu 24,596 wa sekondari hususani Sayansi na Hisabati. 
Hata hivyo, upungufu ulikuwa mkubwa zaidi kabla ya Serikali kuajiri walimu wapya 36,338 mwaka huu.  Kati ya idadi hiyo ya walioajiriwa,  walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati ni 2,364, ngazi ya cheti 17,928, Stashahada 5,416 na Shahada ni walimu 12,994.  
Kawambwa alisema Wizara na wadau wake, itaendelea kuwaandaa kulingana na mikakati na kadri rasilimali zinazohitajika zinavyoendelea kupatikana. 

No comments: