WAKONGO WAFURAHIA UFUNGUZI WA OFISI YA TPA LUBUMBASHIWafanyabiashara wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC), wameelezea na matumaini yao kwa hatua ya Tanzania kufungua ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari (TPA) mjini Lubumbashi, Katanga nchini humo.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao baada ya kuzinduliwa kwa ofisi hiyo hivi karibuni, wafanyabiashara hao wanaopitisha mizigo yao katika Bandari ya Dar es Salaam, wamesema kuanzishwa kwa ofisi hiyo kumekuja wakati muafaka na kuwa itawarahisishia biashara yao.
Mmoja wa wafanyabiashara hao,  Mubanzo Fils anayeendesha kampuni ya ETS Mubanzo, alisema jumuiya ya wafanyabiashara Lubumbashi imefurahia kupata ofisi hiyo wanayotarajia kurahisisha kazi zao na kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili.
“Tuna furaha kubwa kwa hatua hii muhimu,” alisema.
Inatarajiwa tatizo lililokuwa likiwakabili wafanyabiashara hao la kukabiliana na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio waaminifu, sasa itakuwa historia kwa kuwa ofisi ya Lubumbashi itakuwa na orodha ya wakala wanaokubalika na waaminifu.
Pia mienendo ya taarifa za mizigo itafanyika mjini humo na   kuharakisha taratibu za mizigo bandarini hapo.
Kwa upande wake, Lumbu Useni wa kampuni ya Luwang SPRL alitoa mwito kwa wafanyakazi kwenye ofisi hiyo kutimiza lengo lilikusudiwa. “Wafanye kazi kwa bidii na akili zao zote ili lengo lililokusudiwa na nchi hizi lifikiwe na sisi tuweze kufaidika.”
Mfanyabiashara mwingine,  Mohamed Hassan Hammy, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Drill Tek ya mjini humo alisema Kongo ni soko kubwa hivyo Tanzania imefanya busara kubwa kufungua ofisi hiyo.
Mizigo ya DRC inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikiongezeka kwa asilimia takribani 24 kwa mwaka tangu mwaka 2004, kutoka tani 155,611 hadi tani 1,117,249 mwaka 2013.

No comments: