WAJUMBE UKAWA, TANZANIA KWANZA WALUMBANA BUNGENI



Kauli ya Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul (Chadema), aliyoitoa jana kwamba CCM imechoka na haitoshi, ilisababisha kuibuka kwa malumbano kati ya makundi mawili yaliyoundwa ndani ya Bunge Maalumu la Katiba la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Tanzania Kwanza. 
Gekul ambaye ni mjumbe wa Ukawa, akichangia hotuba ya makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema hayo akizungumzia matumizi mabaya ya fedha.
Alisema kuwa Serikali ya CCM imechoka na haitoshi na wananchi wataishughulikia katika sanduku la kura.
Akijibu hoja hizo,  Mbunge wa Sikonge, ambaye ni kiongozi wa kundi la Tanzania Kwanza, Said Nkumba (CCM) alisema Chadema ndio imechoka kutokana na kila mwaka kutafuta ushindi katika uchaguzi bila kuupata. 
“Chama kilichochoka ni kile kinachofanya juhudi kila mwaka kishinde lakini kinashindwa…CCM ni njia kuu hatuwezi kuchepuka,” alisema Nkumba. 
Nkumba alishutumu hotuba iliyotolewa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,  Freeman Mbowe na kusema badala ya kujenga hoja za kisera, alipeleka bungeni hoja ya Katiba ambayo ni hoja ya madaraka. 
Akijibu hoja ya Mbowe katika hotuba yake juu ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali, Nkumba alihoji, “Mbowe ana usafi gani.”
Alikumbushia tuhuma zilizowahi kuwasilishwa bungeni juu ya kiongozi huyo wa upinzani kumwamuru mbunge mmoja wa kike atoke Marekani, alikokuwa katika safari  iliyogharimiwa na posho za Bunge, wakutane Dubai kwa ajili ya masuala binafsi. 
Vile vile Nkumba alisema bungeni kwamba Mbowe alidanganya kwamba hatachukua gari la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani na kusema alilikataa kwa sababu lilikuwa kuu kuu na alipopewa gari jipya, alilichukua. 
“Sasa ile gari tena, katika hali ile ile ya matumizi mabaya kaenda nayo tena Mombasa imekamatwa tena inashukiwa kwamba imebeba mabomu. Hayo hamyasemi hayo, mnazungumza habari za Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake. Acheni michepuko, rudini kwenye njia kuu,” alisema Nkumba. 
Katika hatua nyingine, kitendo cha baadhi ya wabunge kuendelea kukosa uvumilivu katika mijadala inayoendelea bungeni na hivyo kuamua kuzomea, kimekemewa na Spika Anne Makinda akihimiza kila mbunge au upande, kuheshimu mwingine hata kama ataumizwa na hoja zinazotolewa. 
Makinda alikemea  juzi baada ya kuwepo hali ya kuzomeana miongoni mwa wabunge hususani upande wa upinzani dhidi ya CCM, pale
wabunge wa chama hicho tawala walipokosoa  na kujibu sehemu ya  hotuba iliyosomwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe. 
Akiahirisha kikao cha juzi, Makinda alitaka wabunge kujenga utamaduni wa kuvumiliana hata kama kutatolewa hoja ambazo wanapingana nazo, waache wahusika wazungumze. 
Aidha katika kuhakikisha kila mbunge anayechangia anakamilisha dakika zake saba bila kuingiliwa, Spika amedhibiti utaratibu wa wabunge kukatisha wenzao kwa kile ambacho kimezoeleka kuwa ni kutoa taarifa. 
“Kuna wengi walikuwa wakiomba kutoa taarifa wakati mzungumzaji mmoja mmoja anazungumza. Sikuwapa nafasi mpaka saa ya kumaliza. Dakika saba ukimwingilia mtu utavuruga na hautamsaidia. Na taarifa ni yako wewe. Dakika saba  ni chache ukimwingilia atapoteza hoja zake na hataeleweka,” alisema Spika juzi.
Miongoni mwa maeneo ambayo Spika alilazimika kuingilia kati kwa kuwataka wabunge kujenga tabia ya uvumilivu, ni pale Mbunge wa Magomeni, Muhammed Amour Chombo, alipochangia akikosoa hotuba ya Mbowe ambayo pamoja na masuala mengine, ilisema Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alitajwa kuwa siyo raia wa Zanzibar. 
Katika hotuba hiyo ya Mbowe ambayo ilijikita kuzungumzia masuala ya Katiba mpya, alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd katika mkutano wa CCM, alisema Jussa siyo raia wa Zanzibar. 
Alishutumu kwamba kauli hiyo ni ya kibaguzi, kichochezi na yenye kupandikiza chuki dhidi ya jamii ya watu wenye asili ya Kihindi. 
Mbunge Chombo katika kuchangia bajeti hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alikanusha kuwepo ubaguzi dhidi ya Jussa. Alianza kuelezea namna anavyomfahamu Jussa na kueleza Bunge kwamba alisaliti wazee wake. 
Alisema anamfahamu mwakilishi huyo vizuri kuliko Mbowe anavyomwelezea. Akaliambia Bunge kuwa wakati mama yake anaolewa, mbunge huyo Chombo alimshuhudia.
Hata hivyo wakati akiendelea kuchangia, akisema anamfahamu Jussa kuliko wanavyomjua, zilianza kusikika sauti za kuzomea. Spika Makinda aliingilia kati na kuwaambia kwamba kama upande mwingine usingekuwa na uvumilivu, kwa maana ya chama tawala, hotuba ya Mbowe iliyosheheni shutuma kwa Serikali na chama tawala, isingesomwa bungeni humo. 
Mbunge mwingine ambaye  alizomewa  na watu ambao hawakukubaliana na hoja zake,  ni wa Mbinga, John Komba ambaye alisema Chadema na CUF wamekwisha ndiyo maana walisusa Bunge Maalumu la Katiba. 
“Hii hotuba ya Kambi ya Upinzani naichukua tu kama jamaa anapigana na mtu mwenye nguvu kubwa. Amepigwa halafu anasema nishike nitamuua. Chadema na CUF wamemalizwa. Rudini kule tukatwangane kule hapa si sehemu yake. Njooni mpate makonde kule kwenye Bunge Maalumu,” alisema Komba.
Komba aliendelea kuponda vyama hivyo vya upinzani vinavyounda Ukawa akisema, “Hawa sasa hivi watashika mpira kwapani wataondoka...Vumilia yakuingie usishike mpira,” alisema Komba. 
Mbunge wa Dole, Sylvester Mabumba (CCM) alitaka Mbowe aeleze Bunge mantiki ya kusema Tanzania Bara ni mkoloni anayetawala Zanzibar kwa nguvu. “Lakini sifa ya mkoloni huwa anateua gavana. Je gavana aliyeteuliwa Zanzibar ni nani?” Alihoji. 
Naye Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi alisema ingawa anafahamu Bunge  la Bajeti na si la Katiba, yapo mambo ambayo
ameona ni vyema kuyaeleza akisema Mbowe amepotosha Watanzania. “Nilitaka kusimama wakati akitoa taarifa,” alisema Zambi. 
Kwa mujibu wa Zambi, katika hotuba ya Kiongozi huyo wa Upinzani, anatabiria mabaya nchi kwa kusema ikifika uchaguzi bila Katiba, nchi haitaeleweka.
 “Katiba itakamilika saa ngapi wakati nyie mnakimbia mnaenda nje. Lazima mbaki ndani. Sisi sio wa mwisho kuandika Katiba bali ni wananchi,” alisema.
Zambi aliendelea kusema, “Tuache kuaminisha Watanzania kwamba tusipopata Katiba mpya nchi itakwenda vibaya.  Wakati mwingine
viongozi wa Upinzani hawana nia njema na nchi hii. Nchi itakapoingia kwenye vurugu viongozi hawa watakimbia nchi . Tuwe makini na kauli hizi za kupotosha.”
Kwa upande wake, Mbunge wa Tabora Mjini, Aden Rage alisema baada ya Chadema kufanya vibaya katika uchaguzi mdogo wa ubunge Kalenga mkoani Iringa na Chalinze mkoani Pwani, kimeamua kuunda Baraza la Mawaziri Kivuli kwa kushirikisha CUF jambo linalodhihirisha wameshindwa kufanya kazi wenyewe. 
Wakati huo huo Chiligati aliasa Bunge la Bajeti lisigeuzwe kuwa Bunge Maalumu la Katiba.  Alisema hilo ni Bunge la wananchi ambalo wanataka kufahamu juu ya utatuzi wa matatizo yao. 
“Nimeshangaa sana asubuhi hotuba ya kiongozi wa upinzani zaidi ya nusu ya muda amezungumza mambo ambayo yalipaswa yazungumzwe kwenye Bunge la Katiba. Leo zaidi ya dakika 40 akazungumzia mambo ya Katiba badala ya matatizo ya wananchi,” alisema Chiligati.
Akishutumu kitendo cha Mbowe pamoja na wajumbe wengine wa Ukawa kutoka bungeni na badala yake wakaja kutoa maoni kwenye Bunge la Bajeti, Chiligati alisema, “ Badala yake, alichukua timu yake akaweka mpira kwapani akatoka nje…mwezi wa nane (Agosti) timu yake airudishe ndani hayo yote yazungumzwe humu ndani.”

No comments: