WAFUGAJI WATENGEWA MAENEO WILAYA 75 NCHINIHekta 1,349,132 zimetengwa nchini kwa ajili ya ufugaji katika vijiji 543 vya wilaya 75 katika mikoa 21 nchini. Kati ya hekta hizo, hekta 41,027 ziko katika vijiji 18 vya wilaya ya Mbarali.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Saning’o ole Telele alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi (CCM).
Aidha Mbunge huyo alitaka kujua kama Serikali kama iko tayari kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafugaji nchini.
Akijibu swali hilo,  alisema baada ya kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi, halmashauri zitaandaa mipango ya kina ya usimamizi wa maeneo ya ufugaji, itakayobainisha uwezo wa kila eneo kimalisho, miundombinu iliyoko na inayohitajiwa na njia mbalimbali za kuyaboresha ili kuyaongezea tija.
“Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, serikali itaendelea kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji vilivvobaki, kama njia ya kuiongezea tija, kuifanya iwe endelevu na kupunguza migogoro,” alisema.
Aidha, alisema ili uzalishaji wa maeneo hayo uwe endelevu, yatamilikishwa kwa wafugaji mmoja mmoja au kikundi ili kuboresha usimamizi.

No comments: