WAFANYAKAZI WALIOGOMA TAZARA WAGOMA KURUDI KAZINI


Menejimenti ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), imejikuta katika wakati mgumu, baada ya wafanyakazi waliogoma, kukataa kurudi kazini  huku Serikali ikitoa masharti ya kuisaidia.
Mkurugenzi Mkuu wa Tazara, Ronald Phiri jana jioni alikutana na wafanyakazi katika kikao cha dharura, baada ya wafanyakazi hao kugoma kufanyakazi mwanzoni mwa wiki hii, ambapo aliwaomba kurudi kazini, lakini waligoma mpaka pale watakapolipwa mishahara yao ya Februari hadi Mei.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (Trawu), Yasin Mleke alisema mgomo huo unatokana na madai ya mishahara kwa miezi hiyo, ambayo hawajalipwa mpaka sasa na uongozi wa Tazara.
Phiri aliwaambia wafanyakazi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tazara, ameitisha kikao cha dharura cha Bodi, kitakachofanyika kesho kwa lengo la kujadili tatizo hilo la wafanyakazi, ili kulipatia ufumbuzi.
"Ombi kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi na kutoka kwangu, wakati tukisubiri kikao cha Bodi, siku ya Ijumaa turudi kazini, ili majadiliano yatakayofanyika yazae matunda mazuri kwetu…tatizo hili liko kote hata kwa upande wa Zambia," alisema Phiri.
Wafanyakazi walipotakiwa kunyoosha mikono walio tayari kurudi kazini, hakuna aliyenyoosha. Lakini, walipotakiwa kunyoosha mkono ambao hawako tayari kurudi kazini mpaka pale kikao cha bodi, kitakapokaa na kutatua tatizo lao, wote walinyoosha na kusema kuwa hawako tayari kurudi kazini.
Alipotafutwa jana, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka, alisema Bodi ya Wakurugenzi ya Tazara walitoa agizo kupata ufafanuzi ni wapi mishahara ya watumishi 100 wa shirika hilo, ambao ni hewa inapokwenda, na kutaka shirika hilo kutoa taarifa ya fedha walizonazo mpaka sasa.
Aidha, Dk Mwinjaka alisema kuwa mwishoni mwaka jana Bodi hiyo ilitoa agizo kwa Menejimenti kulipa mishahara ya wafanyakazi Februari kwa upande wa Tanzania, jambo ambalo halikufanyika mpaka sasa.

No comments: