WAFANYAKAZI WALIOGOMA TAZARA KUBURUZWA MAHAKAMANIMamlaka ya Reli la Tanzania na Zambia (Tazara) imewapeleka mahakamani wafanyakazi wake waliokuwa wamegoma, wakishinikiza kulipwa fedha zao za mishahara.
Wafanyakazi hao wameendelea kugoma licha ya Serikali  kutoa Sh bilioni 1.6 kulipia mishahara hiyo wiki iliyopita.
Wamegoma kutoa huduma, kwa madai kuwa fedha  hiyo iliyotolewa na serikali ni ya miezi miwili  tu na kwamba umebakia mshahara wa mwezi mmoja.
Akizungumza na mwandishi jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kanda ya Dar es Salaam wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli nchini (Trawu), Yusuph Mandai alisema  menejimenti iliwapeleka Mahakama  Kuu Divisheni ya Kazi,  kwa madai wafanyakazi hao kufanya mgomo kinyume na sheria.
“Ni ukweli kuwa tumeshtakiwa katika mahakama hiyo iliyopo Kinondoni, ambapo Ijumaa  tulipofika shauri hilo liliahirishwa kutokana na maelezo kuwa lilitakiwa kufanyiwa marekebisho,” alisema Mandai. Alisema kuwa hata jana, waliitwa tena mahakamani.
Alisema menejimenti inadai kuwa mgomo huo siyo wa kisheria. Alisema menejimenti hiyo inataka mahakama kutoa amri ya wafanyakazi hao, kurudi kazini. 
Alisema walikwenda tena jana mahakamani kusikiliza shauri hilo.
Katika hatua nyingine, mwandishi alimtafuta Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi,  kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo, ambapo alipokea simu na kudai yuko mkutanoni, huku Msemaji wa Tazara akidai kutokuwapo kazini.
Mgomo wa wafanyakazi  hao, ulianza wiki mbili zilizopita, ambapo walikataa kurudi kazini hadi hapo watakapolipwa fedha yote.
Serikali imeshatoa Sh bilioni 1.6 kwa ajili ya mishahara hiyo, lakini wafanyakazi hao wanadi kuwa ni ya miezi miwili tu, ambapo umebakia mwezi mmoja, ambao fedha yake haijaingizwa katika akaunti ya Tazara, hivyo hawawezi kurudi kazini.
“Fedha inayodaiwa kutolewa bado wafanyakazi hawajaiweka mifukoni, lakini pia bado mwezi mmoja ambao fedha yake hazikuwekwa,” alisema Mandai.
Alisema kuwa ili kuendesha  Tazara kwa ufanisi mkubwa, wafanyakzi hao warudishiwe madaraka.

No comments: