Wabunge wameitaka Serikali kuongeza
uwekezaji katika sekta ya mifugo na uvuvi ili itoe mchango mkubwa katika Pato
la Taifa, huku wakisisitiza kuwa matumizi bora ya ardhi yataepusha migogoro
inayoota mizizi ya wakulima na wafugaji nchini.
Aidha, kwa upande wake, Mbunge wa
Mwibara, Kangi Lugola (CCM), amesema atatema ubunge wake pamoja na kutoa fedha
Sh milioni 50 endapo Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi itamuonesha fedha
za ruzuku zilizotengwa kwa ajili ya wavuvi.
Wabunge hao walikuwa wakichangia bajeti
ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi iliyowasilishwa bungeni juzi na
Waziri Dk Titus Kamani ambaye anaomba Bunge liidhinishe makadirio ya matumizi
ya Sh 66,142,627,000.
Takriban wabunge zaidi ya 15
waliochangia kwa kuzungumza bungeni jana, walisema sekta ya mifugo na uvuvi
inaweza kuisaidia kukuza uchumi wa Taifa na kusaidia sekta nyingine zisizo za
uzalishaji mali kama vile elimu na afya, endapo bajeti yake itaongezwa zaidi.
Lugola katika mchango wake, mbali ya
mambo mengine, alisema, "Waziri amesema atatoa ruzuku kwa wavuvi, lakini
nimetazama katika vitabu vyote sijaona fedha. Ikifika jioni, kama Waziri
atanionesha fungu hilo, nitatema ubunge wangu na nitatoa cheki ya shilingi
milioni hamsini. Maana tumekuwa tunapiga porojo tu."
Mbunge wa Kiteto na Naibu Waziri wa
zamani wa wizara hiyo, Benedict ole Nangoro, alisema kama sekta hizo mbili
zitaongezwa fedha, zitaleta manufaa makubwa, huku akisisitiza Serikali
kusimamia bila upendeleo masuala ya migogoro ya wakulima na wafugaji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kibaha
Vijijini, Hamoud Jumaa (CCM), mbali ya bajeti, aligusia kusuasua kwa ujenzi wa
machinjio ya Ruvu, Mlandizi mkoani Pwani; hoja ambayo pia ilichangiwa na Mbunge
wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM).
Ridhiwani pia alisisitiza matumizi bora
ya ardhi na kutaka kuwekwa kwa sheria ambayo itawalazimisha wafugaji kufuga
kisasa na pia akaomba ujenzi wa majosho ya mifugo.
Mbunge wa Viti Maalumu, Mamelok Sokoine
(CCM), alikuwa na ushauri kwa Serikali kwamba iongeze uwekezaji katika sekta
hizo, itenge matumizi bora ya ardhi, iweke doria katika bahari kuu na kuanzisha
bandari ya uvuvi.
Naye Mbunge wa Kishapu, Suleiman
Nchambi (CCM), alisema mifugo ni dhahabu inayotembea, hivyo akasisitiza
uwekezaji pamoja na elimu kwa wafugaji na wakulima ili kuepusha migogoro kati
ya makundi hayo mawili.
Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo
(UDP), pia alisisitiza suala la elimu kwa makundi hayo mawili, lakini pia
akaiomba Serikali ihalalishe wafugaji watumie maeneo ya ranchi kulisha mifugo
yao badala ya sasa kufanya hivyo kinyemela.
"Wafugaji si masikini kama baadhi
ya watu wanavyotaka jamii iamini hivyo. Tunachohitaji ni kuwaelimisha,"
alisema Cheyo huku akibainisha kuwa Operesheni Tokomeza ilikuwa mbaya na kuwa
suala la kuua mifugo ni lazima likomeshwe.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma
Mjini, Peter Serukamba (CCM), alisema hivi sasa kila mtu anazungumzia masuala
la gesi, lakini akabainisha kuwa hata kama gesi itaanza kuzalishwa nchini,
haitakuwa muarobaini wa matatizo bali kinachotakiwa ni kubadili namna ya
kufikiri kuhusu rasilimali zetu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, alisema uwekezaji kupitia Benki ya
Kilimo inayoanza karibuni, utakuwa mkombozi kwa sekta hiyo, huku akisisitiza
kupima ardhi, kukopa na kuwezesha kama njia ya kuzisaidia sekta hizo.
Mbunge wa Mji Mkongwe, Muhammad Sanya
(CUF), licha ya kulia na bajeti ndogo kwa sekta hizo, aliitaka Serikali kwenda
kusaka masoko ya kondoo Saudi Arabia na Falme za Kiarabu, huku akiahidi
kugharamia tiketi na malazi kwa Waziri kama atashindwa kupata fedha za kwenda
huko.
"Nendeni Saudi Arabia, kuna soko
kubwa la kondoo. Wakati wa hija wanachinja kondoo wengi. Tulitumie hili
kiuchumi. Kondoo wao wanatoa Brazil, mbali kabisa, wakati sisi tuko nao karibu
na pia tunao uhusiano mzuri. Niko tayari kutoa tiketi ya ndege na malazi kwa
Waziri kwenda huko," alisema.
Wabunge wengine, Michael Laizer
(Longido - CCM), Rose Kamili (Viti Maalum - Chadema), Innocent Kalogeries
(Morogoro Vijijini - CCM) na Aeshi Hilary (Sumbawanga Mjini - CCM), pia
walisisitiza uwekezaji, kutengewa kwa maeneo ya wakulima na wafugaji na elimu.
Bunge lilitarajiwa kupitisha makadirio
hayo jana jioni na leo itakuwa zamu ya Wizara ya Kazi na Ajira, kabla ya Bunge
hili la Bajeti kuendelea tena Jumatatu.
No comments:
Post a Comment