WABUNGE WALIOMTUKANA MWALIMU NYERERE SASA WATUBU



Wabunge wanaodaiwa kumkashifu Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere wakati wa Bunge Maalumu la Katiba, wamempigia simu Mama Maria Nyerere kumuomba msamaha, kutokana na maneno ya kashfa ndani ya bunge hilo.
Hayo yamethibitishwa jana na Mama Maria Nyerere wakati akizungumza na  Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na wazalendo wa Tanzania, waliojitokeza kwa wingi kwenda nyumbani kwa mjane huyo wa Baba wa Taifa, Msasani jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mama Maria alisema kuwa hakuweza kumtambua mmoja wa wabunge hao, waliopiga simu, kutokana na yeye kutojua nani aliyemkashifu Baba wa Taifa, kwa kuwa hakuwa akifuatilia mjadala wa bunge hilo.
"Siku moja nilipigiwa simu naombwa msamaha, lakini mimi nikasema ngoja niwaulize wenzangu, waliokuwa wakifuatilia kujua ni nani alimkashifu," alisema Mama maria.
Alisema kwa sasa tayari nchi imeshakuwa na matabaka na ikiwa hakutakuwa na umakini, nchi inaweza ikaingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo ni hatari sana.
Alisema kuwa ikiwa wataendelea kuwakashifu wazee wa taifa hili, nchi haitaweza kufika mbali kutokana na kauli wanazozungumza kuwa ni zenye chuki.
"Nawaambia hata mkizunguka nchi nzima, endeleeni tu, lakini tukirudi nyuma hali ya nchi siyo nzuri na tunapokwenda siyo kuzuri, kiroho nchi imetawaliwa na ibilisi," alisema.
Alisema kinachoonekana kwa sasa nchi ina maadui ndani na nje ya nchi na kwamba silaha pekee ya kupambana nao ni sala, hivyo watu wote kwa ujumla waiombee mema Tanzania.
"Vita inaweza kutokea kwa sababu kila mtu amejiandaa kwa lolote, tukikalia haya tutaumia," alisema.
Akisoma ujumbe wa vijana wenzake, Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Pwani, Mohammed Nyundo alisema kumekuwepo na kampeni yenye nia ovu, iliyoasisiwa hivi karibuni, yenye kuharibu taswira na heshima ya Baba wa Taifa katika jamii na kimataifa.
"Kampeni hiyo inaendeshwa na vibaraka wa nchi za Magharibi na Ulaya, wazandiki na maadui wa amani ya Tanzania, imeendelea kusambazwa kwa kasi na gharama kubwa," alisema Nyundo.
Alisema kutokana na kuwepo kwa kampeni hiyo chafu, jumuiko hilo la vijana wa UVCCM na wazalendo, wameamua kutoa tamko la kulaani na kupinga kwa nguvu zote vitendo vya baadhi ya watu kumtuhumu, kumkebehi na kumtukana Mwalimu Nyerere.
Aidha, alisema kwa masikitiko makubwa, wameshitushwa na kufadhaishwa kwa kuona chombo kikubwa na taasisi muhimu, ambayo ni mhimili wa serikali kama Bunge, linakuwa uwanja wa matusi ya kumtukana mwasisi wa taifa.
"Imefikia wakati sasa kwa Bunge tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kudhibiti na kuondoa kinga yake kwa wale wote, ambao kwa ujinga na kutumika, wameamua kuanzisha na kuendesha kampeni kabambe ya kutia doa taswira na heshima ya Baba wa Taifa," alisema.
Vijana hao zaidi ya 100 walikwenda kumuona Mama Maria ili kufikisha ujumbe wao wa kutaka amani na umoja wa Taifa, viendelee kulindwa. Vijana hao ni kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Katavi, Unguja Kusini, Unguja Kaskazini na Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Vijana hao walisema baada ya kumuona Mama Maria, watakwenda Tanzania Visiwani kwa ajili ya kwenda kumuona Mama Fatma Karume, ambaye ni Mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amaan Karume.
Wakati wa Bunge Maalumu la Katiba likiendelea kati ya Februari 18 na Aprili 25 mwaka huu lilipoahirishwa hadi Agosti 5, mwaka huu ili kupisha Bunge la Bajeti, vyombo mbalimbali viliandika kwa kudai kuwa miongoni mwa wabunge hao ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alimtukana Baba wa Taifa.
Lissu, jana hakupatikana kuzungumzia hilo, kwani kila alipopigiwa kupitia simu yake ya kiganjani, ilikutwa inakatwa badala ya kupokelewa.

No comments: