VYAMA VYA SIASA VYASHINDWA KUTOA TAARIFA KWA MKAGUZI MKUUVyama 10 vya siasa kati ya 21 vyenye usajili wa kudumu, vimeshindwa  kuwasilisha hesabu zao za vyama kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa ajili ya ukaguzi.Kati ya hivyo, vyama 11 havikuwasilisha taarifa zao huku vinne vilivyokaguliwa havina akaunti ya benki.Hayo yalielezwa jana na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa na kuongeza kuwa hakuna chama cha siasa kilichowasilisha tamko la mali zinazomilikiwa na chama.Kwa mujibu wa Utouh, mpaka sasa hakuna chama cha siasa  kilichowasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa tamko la mali zinazomilikiwa na chama husika.Alisema katika ukaguzi huo, alikutana na changamoto nyingi katika ukaguzi wa fedha ambazo si za umma.Mkaguzi huyo alivitaja vyama ambavyo havina akaunti ya benki kuwa ni pamoja na UMD, NLD, NRA na ADC.Alisema kwa sasa utaratibu unafanyika ili kuangalia upya utaratibu wa sheria ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ili kuwezesha vyama hivyo kukaguliwa.
“Kuna baadhi ya vyama havina ruzuku hivyo wakati mwingine unaweza kupata changamoto,’’ alisema.
Akizungumzia hali ya magereza hapa nchini, alisema hivi sasa kuna magereza 122 hapa nchini.
Alisema magereza hayo kwa sasa yanatoa huduma kwa wafungwa 45,000 wakati uwezo wake ni wafungwa 22,669.‘’
Hali hii imeongeza ugumu wa udhibiti na kufuatilia haki za wafungwa kwenye magereza yenye msongamano mkubwa kiasi hicho,’’ alisema.
CAG alisema  katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2013  jumla ya hati 961 za ukaguzi zilitolewa (bila kujumuisha kaguzi maalum 16 na za ufanisi sita ).
Alisema kati ya hati hizo, hati zinazoridhisha ni 816 ambazo ni sawa na asilimia 85, hati za shaka ni 131 sawa na asilimia 13.6, hati zisizoridhisha ni nane sawa na asilimia 0.8 na hati mbaya sita sawa na asilimia 0.6.
“Pamoja na kwamba kuna jumla ya hati mbaya sita na hati zisizoridhisha nane kwa taasisi zote nilizokagua kwa mwaka huu, mwelekeo wa hati za ukaguzi kwa ujumla unaonesha kuimarika kwa utendaji wa Serikali katika kusimamia makusanyo ya mapato na matumizi,” alisema.
Pia alisema kwa mwaka ulioishia Juni 30, mwaka huu hali ya deni la taifa lilifikia kiasi cha Sh trilioni 21.2, ongezeko la trilioni 4.2 sawa na asilimia 25 ikilinganishwa na kiasi cha Sh trilioni 16.9 mwaka 2011/2012 deni hilo linajumuisha deni la ndani na deni la nje.
Alisema hali halisi ya deni la ndani lilifika kiasi cha Sh. trilioni 5.7 kwa mwaka ulioishia Juni 30, mwaka huu ikiwa ni ongezeko la trilioni 1.2 sawa na asilimia 27 kutoka kiasi cha trilioni 4.5 kwa mwaka 2011/01.
Utouh alisema ongezeko hilo lilisababishwa na mikopo kutoka kwa mabenki na wafadhili wa nje, kwa ajili ya kusaidia miradi mikubwa ya maendeleo kama uboreshaji wa miundombinu katika nyanja za usafirishaji, majisafi, mkongo wa mawasilino wa Taifa na bomba la gesi.
Alisema taarifa za misamaha ya kodi kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2013 zimeonesha kiasi cha Sh trilioni 1.5 kilitolewa kama misamaha ya kodi.
Hata hivyo, alisema misamaha ya kodi kwa mwaka ulioishia Juni 30, mwaka 2013 imepungua kutoka Sh trilioni 1.8 mwaka 2011/2012 hadi trilioni 1.5 mwaka 2012/013.
“Ukaguzi wangu pia umebaini mishahara kwa watumishi walioacha kazi, waliofariki, waliostaafu imeendelea kulipwa  kupitia katika akaunti zao,” alisema.
Alisema   Sh bilioni 1.6 na makato ya Sh milioni 497 ziliendelea kupelekwa kwenye taasisi kama Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa, Mamlaka ya Mapato na Mifuko ya Jamii.
Pamoja na hayo, Utouh alitaka serikali kuangalia namna ya kuwekeza katika majengo yake yenyewe kwani ukaguzi ulibaini ofisi 14 za Serikali zililipwa  Sh bilioni 7.9 za kodi ya pango kwa mwaka.

No comments: