VODACOM, CBA WAZINDUA HUDUMA MPYA YA M-PAWAKampuni kinara ya mtandao wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi nchini Vodacom na Benki ya Biashara Afrika (CBA), jana walizindua huduma mpya yenye kuleta mapinduzi makubwa ya M-Pawa itakayowawezesha mamilioni ya watanzania kuhifadhi fedha na kukopa kupitia simu zao za mkononi.
Uzinduzi wa huduma hiyo ulifanyika jana Dar es Salaam, mgeni rasmi akiwa Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati anazindua, alisema; "Uzinduzi wa kihistoria wa M-Pawa kwa kiasi kikubwa ni uthibitisho wa mafanikio yaliyotokana na mageuzi yaliyofanyika kwenye sekta ya fedha nchini ambayo yamechangiwa pamoja na mambo mengine uwekezaji mkubwa katika sekta ya mawasiliano na hivyo kuwawezesha wananchi kumudu kuzifikia huduma za fedha."
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Rene Meza alisema; "M-Pawa ni ubunifu mpya katika sekta ya huduma za fedha ambao unaleta pamoja uzoefu wa zaidi ya miaka 50 wa benki ya CBA katika Afrika Mashariki na mafanikio makubwa ya mtandao mpana wa huduma ya M-Pesa wenye mawakala zaidi ya 65,000 nchi nzima.
“Huduma hii itaimarisha zaidi uletaji pamoja wa huduma za kifedha kwa kuwezesha wananchi kuweka akiba ya hadi Shilingi moja, na kukopa kadiri mteja anavyokidhi vigezo."
Aliongeza kuwa, "M-Pawa ni rahisi kutumia, mteja haitaji kutuma wala kujaza fomu za maombi. Kila mmoja sasa anaweza kufungua akaunti ya benki kwenye benki ya CBA kwa urahisi zaidi kiasi tu cha kuchagua M-Pawa kutoka simu yake ya mkononi katika menu ya huduma ya M-Pesa. Zaidi, haina gharama zozote wala ukomo wa kutoa ama kuhamisha fedha kutoka M-Pesa kwenda M-Pawa na kinyume chake."
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi wa CBA Tanzania, Ndewirwa Kitomari, alisema: "M-pesa ilikuwa ni mbia sahihi kwetu kuifikisha huduma hii Tanzania tukiamini kuwa kupitia mtandao wake mpana na mfumo imara wa  mawakala zaidi ya 65,000 waliosambaa nchi kote, huduma hii itapokelewa na kukua kwa kasi hapa nchini."
Vodacom na CBA wanalenga kuwafikia mamilioni zaidi ya watanzania walio nje ya mfumo rasmi wa huduma za kibenki nchini mbali na wateja milioni 5 ambao tayari kwa sasa wanatumia huduma ya M-pesa.
Mbali na ubia na CBA, M-pesa pia ina ubia wa kibiashara na benki zaidi ya 21 nchini inayowapa uwezo wateja wake kuweka ama kutoa fedha wakati wowote mahali popote kwa urahisi zaidi katika akaunti walizonazo kwenye benki hizo.

No comments: