VITA DHIDI YA UJANGILI SASA NI KIMATAIFA



Tanzania imesaini mikataba minne na Jumuiya za Kimataifa na wadau wa kuhifadhi mazingira, kwa ajili ya kupambana na ujangili na uhalifu wa wanyamapori katika hifadhi na mbuga za wanyama nchini Tanzania.
Mikataba hiyo iliwekwa saini juzi jioni kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Taasisi ya Kimataifa inayosimamia Hifadhi (ICCF-Group), Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Umoja wa Ulaya (EU), Benki ya Dunia na nchi za China, Ufaransa, Ujerumani na Norway.
Mikataba hiyo ni matokeo ya Mkutano wa Kimataifa wa Kuzuia  Uhalifu wa Wanyamapori na kuendeleza Uhifadhi wa Mazingira, uliofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam na kushirikisha viongozi wa Serikali, jumuiya za kimataifa, wafanyabiashara na wadau wengine katika sekta ya utalii na maliasili
Walioshiriki katika utiaji saini ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Kiongozi wa UNDP, Hellen Clerk ambapo mkataba huo ni kwa ajili ya Mfuko wa Pamoja wa Kuhifadhi Mazingira.
Mkataba wa pili na wa tatu, ulisainiwa kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ICCF-Group na UNDP. Mikataba hiyo ni ya makubaliano kuwa Tanzania, ifanye mkutano wa Kanda   Oktoba mwaka huu na mwakani ifanye Mkutano wa Mapitio
ya Utekelezaji ya Makubaliano yaliyotokana na mkutano huo.
Mkataba wa nne ulikuwa kwa ajili ya ushirikiano baina ya Tanzania na washirika wa kimataifa, kupambana na kuzuia uhalifu wa wanyapori na waliotia saini ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na kwa upande wa washirika wa kimataifa walikuwa ni mwakilishi wa UNDP, ADB, Benki ya Dunia na mabalozi wa China, EU, Ufaransa, Ujerumani na Norway.
Akitoa hotuba ya kufunga mkutano huo wa siku mbili, Pinda alisema  kampeni ya kupambana na ujangili Tanzania na nchi zilizoathiriwa, haiwezi kufanikiwa ikifanya peke yake, kwani hilo ni tatizo la dunia linalohitaji dunia nzima kushirikiana.
Pinda alisema zinahitajika juhudi za pamoja, kukabiliana na tatizo hilo katika maeneo  wanakoishi na wasikoishi tembo nchini na katika bara la Afrika. 
Alishukuru wadau wa kimataifa kwa kushiriki mkutano huo na kuomba washirika wa ndani na wa kimataifa, kufanya kazi na Tanzania kukabiliana na tatizo hilo la ujangili na biashara haramu ya wanyamapori na kusisitiza suala la kuharibu mitandao ya majangili.
Pinda alisema mkutano huo, unadhihirisha  urafiki na ushuhuda wa namna wadau wote walivyojizatiti kwa ajili ya uhifadhi endelevu na kwamba kampeni ya kupambana na ujangili, inahitaji kuwa endelevu mpaka mwisho ushindi upatikane.
Waziri Mkuu aliahidi washirika na marafiki wa Tanzania katika mapambano dhidi ya ujangili, kuwa Serikali itatumia msaada wowote, uliotolewa kwa ajili ya kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo, kwa ajili ya kuzuia ujangili na biashara haramu ya wanyamapori.
"Kwa kuwa kazi bado ni kubwa mbele, nachukua nafasi hii kuomba wadau wote wa ndani na wa nje, kuendelea kusaidia juhudi za Tanzania kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori," alisema.
Mkuu wa UNDP, Hellen Clerk alizitaka serikali duniani kote kuongeza mapambano dhidi ya ujangili wa tembo na biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori kama meno ya tembo.
Clerk alisema uhalifu unaotokana na biashara ya pembe za ndovu, una madhara makubwa kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu katika nchi zinazoendelea kwa kuliibia Taifa utajiri wake, kuharibu maliasili kwa ajili ya kizazi kijacho, kuchochea uhalifu, rushwa na kudhoofisha usalama wa jamii na taifa.
"Vitendo hivi vya uhalifu vinawaweka wanawake, watoto na wengina katika hali ya umasikini na maisha magumu na yaliyo na hatari," alisema.
Clerk alisema sheria zenye nguvu na zinazotekelezeka zinahitajika, ili kupunguza mahitaji ya bidhaa haramu za wanyamapori na jamii kufanya shughuli za kujiimarisha na kujipatia kipato Tanzania na nchi zingine zenye tembo na wanyamapori.
Alisema shirika lake limejizatiti kusaidia juhudi za kupambana na biashara ya wanyamapori kwa kusaidia utawala bora, utekelezaji wa Sheria, kupunguza umasikini na kulinda mazingira kwa kushirikiana na serikali na washirika wengine.
"Uimarishaji wa utawala bora ni muhimu katika kukabiliana na biashara haramu ya pembe za ndovu na utekelezaji wa sheria unapaswa kufanywa katika eneo husika na kuimarisha mfumo wa kitaifa," alisema.
Nyalandu alisema ni kazi kubwa, kukabiliana na magenge ya majangili na hivyo kuna mahitaji mkubwa wa msaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na washirika wengine.
"Haya makundi yapo hapa, kwa sababu kuna mahitaji ya bidhaa hizo kutoka nchi nyingine. Kwa hiyo ni suala la dunia nzima kushirikiana na kuhakikisha makundi haya yanatokomezwa kabisa na biashara hii inaondolewa kabisa," alisema na kuongeza kuwa Serikali iko madhubuti kuhakikisha inafanya kila iwezalo kuzuia ujangili.

No comments: