VINASABA VYASAIDIA SERIKALI KUVUNA BILIONI 33.53/- SEKTA YA MAFUTA


Vitendo vya uchakachuaji mafuta vimeweza kudhibitiwa na kuiwezesha serikali kupata mapato ya Sh bilioni 33.53 tangu Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA) ilipochukua hatua ya kudhibiti mwenendo wa sekta ndogo ya mafuta ya petroli. 
Ripoti ya Matokeo ya Kifedha yatokanayo na hatua za EWURA kudhibiti sekta ndogo ya mafuta ya petroli ilitolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuzinduliwa juzi, imebainisha kuwa tatizo la uchakachuaji wa mafuta limedhibitiwa baada ya EWURA kudhibiti hali hiyo kwa kuweka vinasaba. 
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyowasilishwa na Dk Haji Semboja aliyeongoza uchunguzi huo, ilisema kutokana na kuwekwa vinasaba katika kipindi cha miaka mitatu serikali ilifanikiwa kupata mapato kiasi cha Sh bilioni 33.53. 
Ripoti hiyo pia inaonesha tangu EWURA ifanikiwe kudhibiti mafuta kuuza njiani, mapato yameongezeka kutoka Sh bilioni 146.5 mwaka 2010/2011 na kufikia Sh bilioni 192.2 kwa mwaka 2012/2013 wakati mapato yaliyotokana na kuingiza mafuta kwa pamoja yalikuwa Sh bilioni 121.7. 
Hata hivyo pamoja na EWURA kufanikiwa udhibiti katika sekta hiyo, Dk Semboja alipendekeza kudumishwa na kuboreshwa mfumo wa kuweka vinasaba ili kuzuia uchakachuaji na pamoja na EWURA na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya kazi kwa pamoja. 
Katika kuzuia uuzaji mafuta njiani, ripoti imependekeza EWURA kufanya kazi kama Bodi ya Udhibiti Huru na kuongeza sekta ya petroli inatakiwa kuchukuliwa kwa umuhimu wake, kwani inachangia katika maendeleo na uboreshaji wa miundombinu. 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akizindua ripoti hiyo alisema ripoti hiyo imeweka wazi namna EWURA ilivyofanikiwa kutekeleza majukumu yake kwa kiwango ambacho serikali iliyatarajia na kwamba imefanya vizuri katika ushindani kwa kufanikisha bei ya mafuta kuwa ya kutabirika na kufanya mafuta kuwa yenye ubora na kuaminika. 
“Tangu tuanze mtindo wa kuagiza mafuta kwa pamoja, utaratibu huu umeiwezesha serikali kupata mapato zaidi na biashara ya mafuta nchini imeongezeka,” alisema. 
Katika hatua nyingine, Muhongo aliitaka EWURA kutumia muda mfupi kujadiliana na kufanya maamuzi nyaraka za wawekezaji katika sekta ya nishati na kwamba katika juhudi za kuinua uchumi na kuondokana na umasikini hauhitajiki urasimu.

No comments: