VIJIJI 12 MBEYA KUPATIWA HUDUMA YA UMEMESerikali inatarajia kutumia  Sh bilioni 1.2 kwa ajili ya utekelezaji wa  mradi wa umeme katika vijiji 12 vilivyopo mkoani  Mbeya.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga aliliambia bunge jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema).
Mbunge huyo alitaka kujua  ni lini serikali itapeleka umeme katika Kata za Iduda, Isyesye, Itende, Tembela, Mwansanga, Mwansekwa na Iziwa vilivyopo Jijini Mbeya, ambapo wananchi walishaweka waya kwenye nyumba zao kwa zaidi ya miaka minane.
Akijibu swali hilo, Kitwanga alisema miradi ya kupeleka umeme kata ya Iduda, Mwansekwa na Iziwa imejumuishwa katika miradi ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) ya kupeleka umeme katika maeneo ya Iduda, Igawilo, Itagha, Hasanga, Iwambala, Itanji, Utukuyu, Mwasenga, Itengano na Iziwa.
Alisema miradi hiyo itajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 16.5, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 11 yenye urefu wa kilomita 13, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 26.
Pia, alisema fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kufunga transfoma tano na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 2,335.

No comments: