VIGOGO WALIOTIMULIWA MALIASILI WAREJESHWA

Vigogo wa Wizara ya Maliasili na Utalii, waliotimuliwa kazi hivi karibuni na Waziri Lazaro Nyalandu, wamerejeshwa kazini.
Taarifa za ndani ya Wizara zilizofikia gazeti hili jana, zilieleza kuwa vigogo hao, Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Jafari Kidegesho, walikabidhiwa barua za kurejea kazini jana.
Mwandishi alimtafuta Msemaji wa Wizara hiyo, Nurdin Chamuya ambaye hakukanusha wala kukubali kuhusu hatua hiyo, na badala yake alisema alikuwa katika kikao tangu asubuhi hivyo apewe muda amtafute Katibu Mkuu, Maimuna Tarishi.
Baada ya muda, Chamuya aliwasiliana na mwandishi na kusema kuwa ameshindwa kuwasiliana na Katibu Mkuu, kwa kuwa yuko katika vikao vya Bajeti na hivyo atatoa taarifa kama suala hilo lipo baadaye.
Nyalandu alimuondoa Profesa Songorwa katika nafasi ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Alisema amechukua hatua hiyo kutokana na kutokuridhishwa  na utendaji wa kazi wa idara hiyo katika mapambano dhidi ya ujangili yanayoendelea nchini.
“Utekelezaji wa agizo hili unaanza mara moja, nami namteua Bwana Paul Sarakilya kukaimu nafasi hiyo ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzia sasa.
“Aidha, ninamuondoa Profesa Jafari Kidegesho katika nafasi ya Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori na kumteua Dk  Charles Mulokozi kuchukua nafasi hiyo,” alisema Nyalandu wakati akitangaza hatua hiyo.  
Taarifa zaidi zimeeleza kuwa watendaji wote waliokaimishwa nafasi za vigogo hao wamepewa barua na Katibu Mkuu   kurejea kwenye nafasi zao za zamani. 
Mwandishi alimtafuta Katibu Mkuu, lakini simu yake iliita bila majibu huku simu ya Nyalandu ikikosekana.

No comments: