'VIBABU' KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA KULAWITI WATOTO SITA



Wazee wawili akiwemo mlinzi mmoja wa ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya wilaya ya Bunda, mkoani Mara, wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kulawiti wanafunzi sita wa shule za msingi zilizoko wilayani hapa.
Waliofikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda, ni pamoja na Thomas Machugu (72) ambaye ni mlinzi  na mkazi wa mtaa wa Saranga, mjini hapa.
Mwingine ni Salum Mfumbasi (66) ambaye ni mfanyakazi wa ndani kwa mfanyabiashara mmoja wa mjini Bunda.
Watuhumiwa hao walifikishwa jana katika mahakama hiyo mbele ya hakimu, James Manota na kusomewa mashitaka yao na mwendesha mashitaka wa polisi Masood Mohammed.
Akiwasomea mashitaka yao, Mohammed alisema washitakiwa hao wote kwa pamoja waliwalawiti wanafunzi hao, ambao umri wao ni kati ya miaka 10 na 13 kwa tarehe na muda tofauti, katika maeneo mbalimbali mjini hapa.
Alisema kuwa polisi waliwagundua watu hao baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema na kwamba baada ya kuwahoji watoto hao walisema kila kitu jinsi washitakiwa hao wamekuwa wakiwaingilia kwa zamu, pindi wanapokwenda shuleni baada ya kupita katika maeneo hayo.
Aidha, aliongeza kuwa baada ya watoto hao kupelekwa hospitalini na kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu ilibainika kuwa walikuwa wamekwishaharibiwa sehemu zao za siri.
Washitakiwa wote kwa pamoja wamekana mashitaka yao na kupelekwa mahabusu hadi Mei 22 mwaka huu, kesi yao itakapotajwa tena mahakamani hapo.

No comments: