UTURUKI YAELEZWA FURSA ZA UWEKEZAJI ZILIZOPO TANZANIA


Raia wa Uturuki wenye mitaji wamehimizwa kuchangamkia fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana Tanzania.
Mwito huo ulitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini hapa iliyoanza juzi Alhamisi.
Katika ziara hiyo, Waziri Membe alionana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kitaifa wa Serikali ya Uturuki akiwemo Waziri Mkuu, Recep Tayyip Erdogan; Naibu Waziri Mkuu, Emrullah Isler; Waziri wa Mambo ya Nje, Ahmet Dovutoglu na Waziri wa Uchukuzi, Lutfi Elgan.
Aidha, Waziri Membe na mwenyeji wake, Dovutoglu walifanya mkutano wa pamoja na waandishi habari na pia kushiriki chakula cha mchana na wafanyabiashara wakubwa wa Uturuki. 
Baadhi ya maeneo aliyoyataja Waziri Membe ni pamoja na sekta ya usafiri wa anga. Alihamasisha Shirika la Ndege la Uturuki kuangalia uwezekano wa kuingia ubia na Shirika la Ndege la Tanzania. 
Aidha alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika viwanda vya nguo, mbolea, gesi, zana za kilimo, miundombinu ya umwagiliaji, umwagiliaji wa matone  pamoja na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, nyama na maziwa. 
Kwa upande wao, Viongozi wa Uturuki walimhakikishia Waziri Membe kuwa watawahamasisha wafanyabiashara wa Uturuki kuwekeza Tanzania.

No comments: