Ubalozi
wa Uturuki kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, wana mpango wa kujenga
kijiji nchini kwa ajili ya kutunza albino wapatao 500.
Ujenzi
wa kijiji hicho unakadiriwa kugharimu dola za kimarekani milioni tano
sawa na Sh bilioni 8.2.
Mke
wa Balozi wa Uturuki, Yesim Meco alisema hayo jana Dar es Salaam kwenye mkutano
na waandishi wa habari, ambao mumewe, Ali Davutoglu alikuwa akizungumzia ujio
wa meli ya jeshi la nchi yake wiki ijayo.
Yesim
alisema lengo kubwa la kujenga kijiji hicho ni kusaidia watu hao wenye
albinism.
Alisema
kabla ya kuanza mchakato wa ujenzi wa kijiji hicho alifika mkoani Shinyanga
iliko kambi yao na kukuta watu hao wakiwa na hofu kuu.
Alisema
aliomba Serikali ya Tanzania kuhamishia kambi hiyo jijini Dar es Salaam ,
ambapo ndipo ofisi za Ubalozi huo zilipo ili kuweza kuwasaidia zaidi.
“Tunamshukuru
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutusaidia eneo la Bagamoyo
ambapo tutajenga kijiji kwa ajili ya kuwasaidia watu hao kuweza kuyafurahia
maisha na uhai wao pia,” alisema Yesim na kuongeza kuwa ujenzi huo unaratibiwa
na Taasisi ya Msaada ya Uturuki na Tanzania (TTAF).
Alisema
katika kijiji hicho, kutakuwa na sehemu ya ufundi wa cherehani, bustani ya
wanyama na shule ya ufundi ambapo watawafundisha wahusika jinsi ya kujipatia
kipato katika maeneo mbalimbali.
Yesim
alisema lengo ni kuwezesha kundi hilo kuishi sehemu salama ambayo itakuwa ya
kisasa na eneo hilo litakabidhiwa kwa chama cha watu wenye albinisim kwa
ajili ya kuliendesha.
Kuhusu
ziara ya meli, Balozi Ali alisema watakaofuatana nayo, watakuwa na shughuli
mbalimbali nchini, kama vile kutembelea kituo cha watoto yatima na shule ya
watu wenye mahitaji maalum.
Alisema
ziara ya meli hiyo, inaanzia Magharibi mwa Afrika ikitoa mafunzo katika
bandari 29 za nchi za Afrika. Inapinga uharamia na kuchangia katika
usalama wa ukanda wa Bahari ya Hindi.
No comments:
Post a Comment