UPANDISHAJI VYEO WAUGUZI WATAKIWA KUREKEBISHWA



Rais Jakaya Kikwete, ameagiza utaratibu wa upandishaji wa vyeo kwa wauguzi, urekebishwe ili wenye sifa wapate stahili zao huku akikemea tabia ya baadhi ya viongozi wenye tabia ya kuwanyima wafanyakazi haki zao.
Rais Kikwete alisema hayo jana jijini hapa, wakati wa maadhimisho  ya Siku ya Wauguzi Duniani, yenye kaulimbiu isemayo ‘Wauguzi ni Nguvu ya Mabadiliko na Rasilimali Muhimu kwa Afya’, yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Shekhe Amri Abeid.
Alisema ni vyema mfumo huo ukarekebishwa, ili wauguzi wanaojiendeleza wapande vyema na kuwashangaa baadhi ya watendaji wenye tabia ya kutowapandisha vyeo watumishi wao, kwa kuhofia nafasi zao kuchukuliwa na wanaojiendeleza.
Mbali na vyeo, Rais Kikwete alisema pia Serikali itatoa ufadhili  kwa wanafunzi wanaosomea Shahada ya Uuguzi nchini ili kuongeza nafasi ya kuwa na wataalamu wengi wenye sifa za kuwahudumia wagonjwa kwa moyo wa huruma.
Alionya kuhusu tabia ya baadhi ya wauguzi wenye tabia ya kutoa lugha za dharau na kejeli kwa wagonjwa na kusisitiza kuwa uuguzi ni wito, hivyo ni vyema wenye tabia hiyo,  wabadilike na kuanza kutumia lugha za kufariji wagonjwa.
Alisema Serikali itaendelea kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwenye zahanati, wilaya, mkoa pamoja na kusambaza vifaa tiba na kuongeza idadi ya watumishi.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kwebwe  Stephen Kebwe, alisema utafiti wa idadi ya watu duniani unaonesha kuwa katika afya kwa mwaka 2010/2013, kumekuwa na ongezeko la uelewa wa matumizi ya njia za uzazi wa mpango  kwa asilimia 96 na kwa wanawake na wanaume asilimia 97.
Pia alisema vifo vya watoto navyo vikipungua kutoka vifo 165 kwa vizazi hai 1,000 kwa mwaka 1990 hadi kufikia 54 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2013.
Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania,  Paulo Magesa aliiomba Serikali kuwaboreshea posho wauguzi, ikiwemo fedha kwaajili ya sare za kazi na kuwapa nyumba, ili watumishi hao wawahi kutoa huduma bora kwa wagonjwa sehemu mbalimbali.

No comments: