UNDP YATOA DOLA MILIONI 22 KWA AJILI YA UCHAGUZI MKUU



Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), limetenga dola za Marekani milioni 22 kwa ajili ya kuunga mkono utoaji elimu kwenye uchaguzi mkuu ujao nchini.
Kiongozi wa shirika hilo, Helen Clark aliuambia Umoja wa Wanawake Wabunge jana mjini hapa kwamba fedha hizo zitatolewa chini ya Mradi wa Uchaguzi unaoendeshwa na shirika lake.  
Alisema shirika lake limepokea maombi kutoka vyama vya siasa kuomba kuungwa mkono hususani kwenye suala la elimu, kujenga uwezo na uhamasishaji katika shughuli za uchaguzi mkuu ujao.  
Alisema fedha hizo zitajikita katika kuelimisha na kuhamasisha wanawake na vijana kujihusisha kwenye mchakato wa uchaguzi huo hususani kugombea nafasi za uongozi.  
Kiongozi huyo wa UNDP alipongeza Tanzania kwa hatua iliyofikia katika kutekeleza malengo ya maendeleo ya millennia; hasa malengo namba moja, sita na saba.  
Alisema pia Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika juhudi za kutokomeza umasikini, kuimarisha afya kwa watoto na kuwezesha watoto kuendelea na masomo hadi sekondari.  
Juhudi nyingine ambazo kiongozi huyo amepongeza Tanzania, ni kupunguza vifo kwa wajawazito na mapambano dhidi ya Ukimwi.  
Kiongozi huyo ambaye anashika nafasi ya tatu kicheo katika Umoja wa Mataifa, baada ya Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, aliendelea kupongeza juhudi zinazofanywa na serikali katika kuwezesha wanawake kisiasa na kwenye utawala.  
Alisema uwepo wa viti maalumu umewezesha idadi kubwa ya wanawake  kuingia kwenye bunge ambalo ni chombo muhimu cha kutunga sheria.  
Wakati huo huo, akiwa ameongozana na Mwakilishi wa UNDP nchini, Philippe Poinsot, kiongozi huyo mkuu wa shirika pia alisifu juhudi za serikali katika kukabili ujangili.  
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake, Anna Abdallah aliambia ujumbe huo kwamba wakiungwa mkono na wadau wengine, wamekuwa wakifanya uhamasishaji  wa wanawake kuingia kwenye
siasa.  
“Tunahamasisha wanawake na kuwajengea uwezo wa kushiriki katika mchakato wa uchaguzi kwa  kugombea nafasi mbalimbali,” alisema.  
Aidha, Clark ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa  New Zealand kwa muda mrefu kabla ya kuingia UNDP, alifanya mazungumzo na Spika Anne Makinda kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam jana.

No comments: