UCHAFU WA MAZINGIRA WAPOTEZA SHILINGI BILIONI 301

Tanzania inapoteza jumla ya shilingi bilioni 301 kila mwaka kama gharama ya kukabiliana na madhara ya uchafu wa mazingira.
Hayo yalisemwa jana na Meneja wa Mradi wa Usafi wa Mazingira Tanzania (UMATA), Kornel Kema wakati akizungumza kwenye mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya usafi wa mazingira iliyofanyika Dodoma.
Huku akinukuu ripoti ya Benki ya Dunia ya Programu ya Usafi wa Maji na Mazingira iitwayo ‘Madhara ya Kiuchumi yatokanayo na hali duni ya usafi wa mazingira Afrika’, Kema alisema kuwa fedha hizi ni nyingi na kwamba zingeweza kuokolewa kama usafi wa mazingira ungeboreshwa nchini.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jumla ya Watanzania  milioni 26 wanatumia vyoo duni na pia zaidi ya watu milioni tano hawana choo na kwamba wanajisaidia haja ndogo na kubwa kwenye maeneo ya wazi.
Pia inaonesha kuwa mtu mmoja asiye na choo bora hupoteza muda wa siku mbili na nusu kwa mwaka katika kutafuta eneo la kujisaidia katika maeneo ya wazi ili watu wengine wasimuone.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na mradi wa UMATA yalifunguliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa.
Kwa mujibu wa Mkwasa alisema pamoja na kwamba Dodoma ina matatizo makubwa ya upatikanaji wa maji lakini hilo lisiwe kisingizio cha kutotilia maanani usafi wa mazingira.
“Hatuwezi kuacha wananchi wasijali usafi kwa vile kuna tatizo la maji, usafi wa mazingira si kuoga tu ni usafi wa jumla katika kaya na hata kuhakikisha kuna choo bora,” alisema.
Alisema Wilaya ya Bahi ilianza kampeni ya usafi wa mazingira muda mrefu na wametenga kila Jumatano kuwa siku ya usafi na hakuna duka linaloruhusiwa kufunguliwa bila usafi kufanyika.
Pia alisema Wilaya hiyo imefanikiwa kuhamasisha wafugaji 60 wenye mifugo mingi wameuza mifugo yao na kujeng nyumba na vyoo bora, wamechimba visima vya maji na hata kupeleka watoto wao shuleni.
Ofisa Afya wa Mkoa wa Dodoma, Edward  Ganja alisema  katika mkoa wa Dodoma  asilimia 27.9 ya kaya zina vyoo visivyo bora na asilimia 72 ni kaya ambazo hazing vyoo bora.

No comments: