TUCTA YALALAMIKIA UTITIRI WA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMIIShirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) nchini limependekeza kuwepo kwa mifuko miwili ya hifadhi za jamii ili kupunguza gharama kubwa ya kuiendesha na kwamba gharama hizo ziingizwe kwenye mafao ya wastaafu.
Hayo yalielezwa juzi na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Nicholas Mgaya wakati akifungua semina juu ya elimu ya Mifuko ya Hifadhi iliyoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi na Mdhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).
“Tanzania inaonyesha ndio yenye mifuko mingi ya hifadhi za jamii ukilinganisha na nchi jirani za Kenya, Uganda na Zambia ambapo imekuwa ikitumia gharama kubwa katika kuiendesha, bora fedha hizo za uendeshaji zielekezwe katika kuboresha mafao ya wastaafu,” alisema.
Alisema ombi la Shirikisho la Wafanyakazi kwa Mamlaka ya SSRA na Serikali ni kuwepo kwa mifuko miwili ya hifadhi za jamii ambapo mmoja utahusisha sekta binafsi na mwingine watumishi wa umma ili kupunguza gharama za kuendesha mifuko hiyo.
Alisema imefika wakati sasa washirikiane na SSRA ili waone ni namna gani wanaweza kufanya mabadiliko hayo kwa kupandisha hesabu za ukokotoaji kwa mifuko ya hifadhi ambayo ipo chini badala ya kushusha ile yenye kiwango cha juu.

No comments: