TEMBO WAUA BAADA YA KUVAMIA MAKAZI KARIBU NA MJI WA DODOMAWatu wawili wakazi wa Kitongoji cha Kawawa, Manispaa ya Dodoma wamekufa baada ya kukanyagwa na tembo wenye hasira jana.
Taarifa  iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime watu hao aliwataja kuwa ni Elizabeth Magawa (80) na Geofrey Mwalabule (7) mwanafunzi anayesoma darasa la pili  Shule ya Msingi Mpunguzi.
Akifafanua tukio hilo Kamanda Misime alisema kwamba  majira ya saa 4 asubuhi jana, tembo wanane, wakubwa wakiwa saba waliingia katika Kijiji cha Mpunguzi kilichopo kiasi cha kilomita 20 kutoka Dodoma mjini barabara ya kwenda Iringa.
Alisema walipoingia tembo hao walianza kula mazao yaliyopo shambani mtama na uwele hali iliyowafanya wanakijiji  waitane na kukusanyika kwa lengo la kuwafukuza tembo hao.
Anasema wananchi hao bila kutafuta msaada wa watu wa Mali ya Asili waliwapigia kelele tembo hao na kuwatupia mawe hali iliyowafanya wakasirike na kucharuka.
Katika hali hiyo tembo hao waliwakanyaga watu wawili katika Kitongoji cha Kawawa na kuwaua kisha wakatokomea wakimuacha tembo mtoto.
“Tembo huyo mtoto kwa sasa analindwa na watu wa Mali Asili akifanyiwa utaratibu wa kurejeshwa kunakohusika,” alisema Kamanda Misime.
Aidha Kamanda Misime amesema kwamba juhudi za kutambua tembo hao wametoka mbuga gani zinaendelea.
Amewataka wananchi wanapoona tembo au makundi yao watoe taarifa Polisi au Mali Asili na waache kuwapigia kelele au kuwapiga kwa vitu vyovyote kwani wanaweza kucharuka na kuleta madhara zaidi.

No comments: