TANZANIA YASIFIWA KUFUNGUA OFISI YA TPA LUBUMBASHI



Serikali ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC), imesifu hatua ya Tanzania kufungua ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari (TPA), kwamba ni ya kizalendo na inayothibitisha uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni baada ya uzinduzi wa ofisi hiyo mjini Lubumbashi, Waziri ya Uchukuzi wa Jimbo la Katanga, Kahozi Sumba, alisema ufunguzi wa ofisi hiyo, utarahisisha na kuleta ufanisi katika kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara wa Kongo wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam,  na pia utasaidia kuboresha maisha yao.
"Kurahisisha biashara ina maana ya kupata maendeleo na kuboresha maisha yetu, tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa uamuzi huu," alisema baada uzinduzi huo, uliofanywa na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe.
Sumba alisema Serikali ya nchi hiyo, inatarajia kuwa wafanyabiashara wa Kongo sasa hawatakumbana tena na changamoto walizokuwa wanakabiliana nazo awali katika biashara zao kati ya Kongo na Tanzania kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Alihimiza Jumuiya ya Wafanyabiashara wa nchi hiyo, kuthibitisha kuwa kweli walikuwa wanaihitaji ofisi hiyo kwa kuitumia kutatua matatizo yao.
"Thibitisheni kwa vitendo kuwa kweli mlikuwa mnaihitaji ofisi hii," aliwaambia baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa katika uzinduzi huo.  
Awali, akizungumza kwa niaba ya Gavana wa Jimbo la Katanga, Moise Katumbi, Naibu Gavana wa jimbo hilo, Yav Guilbert alimmwagia sifa Mwakyembe, akisema amethibitisha kuwa ni mtu wa vitendo.
Katika ziara yake Machi mwaka huu mjini Lubumbashi, Mwakyembe aliahidi kuwa ofisi hiyo ingekuwa tayari mwishoni mwa Aprili, jambo ambalo limetekelezwa kwa wakati.
"Waziri Mwakyembe si aina ya wanasiasa wanaotoa ahadi za uongo na ameonyesha kuwa Tanzania inaweza kuileta Afrika pamoja na kupata maendeleo," alisema.
Awali, Dk Mwakyembe alisema kuwa ofisi hiyo mpya itasaidia wafanyabiashara wa DRC, kumaliza matatizo yao Lubumbashi badala ya kusafiri hadi Dar es Salaam.
"Wataweza kufanya malipo ya bandari wakiwa Lubumbashi na kuepuka hatari ya kusafiri na kiwango kikubwa cha fedha na kuibiwa," alisema Mwakyembe.
Alisema tatizo lililokuwa linawakabili wafanyabiashara hao la kukabiliana na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio waaminifu, sasa litakuwa historia kwa kuwa ofisi ya Lubumbashi itakuwa na orodha ya wakala, wanaokubalika na waaminifu.
Pia, mienendo ya taarifa za mizigo, itafanyika mjini humo na hivyo kuharakisha taratibu za mizigo bandarini hapo.
Waziri Mwakyembe alisafiri kwa barabara kutoka Dar es Salaam hadi Lubumbashi kupitia Zambia zaidi ya kilometa 2,000  ili kupata taarifa za changamoto wanazokumbana nazo wafanyabiashara wa DRC, kuanzia bandarini Dar es Salaam hadi njiani wanaposafiri.

No comments: