TANI 80,000 ZA MAHINDI ZAVUSHWA KIMAGENDO KENYA

Zaidi ya tani 80,000 za mahindi zinadaiwa kusombwa kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda nchi jirani ya Kenya kupitia mpaka wa Sirari wilayani Tarime kwa kutumia vibali, vinavyodhaniwa kuwa ni vya kughushi.
Baadhi ya watumishi wa umma, wamedaiwa kutoza ushuru malori yanayobeba mahindi hayo, lakini bila kutoa stakabadhi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika maegesho la malori yaliyopo mji mdogo wa Sirari, baadhi ya watoa habari wetu walisema kwa siku zaidi ya malori 300 yaliyosheheni mahindi, huvuka kwenda Kenya.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, alisema kutokana na kushamiri kwa biashara hiyo, baadhi yao wamekuwa wakitumia vibali bandia.
“Kuna  baadhi ya wafanyabiashara wenzetu ambao sio waaminifu ambao kwa wakati huu  wamekuwa wakisafirisha nafaka kupitia mipaka hii kwenda nchini Kenya wakipita njia za panya na wengine hutumia vibali vya miezi miwili kusafirisha mahindi kwenda Kenya.
Wanatumia mipaka ya Sirari, Kubiterere, Gosebe, Ikoma, Kogaja na Borega kwenda Kenya, hali inayochangia kutopatikana kwa takwimu sahihi kwa chakula kinachotoka nje ya nchi,” alisema.
Mfanyabiashara mwingine alisema kuwa, ”tumekuwa tukitozwa kila lori shilingi elfu 40, ambazo tunalipa bila stakabadhi katika Ofisi ya Idara ya Kilimo iliyopo kituo hicho cha Forodha, tunasikitishwa na kitendo hicho cha ofisi za serikali kutoza ushuru bila ya kutoa stakabadhi hali inayotia shaka.
Tunahisi fedha nyingi zinazokusanywa zinaishia mifukoni mwa watumishi hawa na wengine wako Sirari kwa zaidi ya miaka kumi sasa,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Athuman Kalama hakupatikana kuzungumzuia tuhuma hizo za watumishi wa idara ya kilimo, kutoza ushuru bila kutoa stakabadhi.

No comments: