TABIANCHI NA MUINGILIANO UMESABABISHA HOMA YA DENGUE



Serikali imesema mabadiliko ya tabia nchi pamoja na mwingiliano wa safari yamesababisha kuwepo kwa ugonjwa wa dengue nchini ambapo hatua mbalimbali za kukabiliana nao zimechukuliwa.
Kufuatia hali hiyo serikali imewahakikishia wananchi kuwa hakuna atakayekufa kwa ugonjwa huo kwa kukosa tiba iwapo atakayeona dalili atafika hospitali na kupatiwa matibabu mara moja.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Kebwe S Kebwe wakati akizindua upya kampeni ya Nyota ya Kijani  kwa Kanda ya Ziwa uliofanyika katika uwanja wa Nyamagana.
Katika kukabiliana na ugonjwa huo, Naibu Waziri huyo ameutaka uongozi wa mkoa kushirikiana na Sumatra kuhakikisha wanapuliza dawa kwenye vyombo vyote vya usafiri zikiwemo meli.
Alisema dawa za upuliziaji zimesambazwa kwenye halmashauri zote katika kukabiliana na ugonjwa huo ambao hutokana na virusi baada ya ya kuumwa na mbu aina ya aedes ambao wengi tulizoea kuwa mbu huyo huambukiza homa ya njano.
Alisema ugonjwa huo uliingia nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2010 ambapo watu 40 waliugua lakini idadi hiyo imeongezeka mwaka 2013 kulikuwa na wagonjwa 143 na hii inaonesha mazalia ya mbu hao yameongezeka.
Alisema kuna aina tatu za ugonjwa wa dengue ambapo aina ya kwanza alisema ni ile ambayo huambatana na homa kali na maumivu ya viungo ambapo asilimia 90 ya watu wamekuwa wakiumwa.
Alisema aina ya pili ya ugonjwa huo ni ule kutokwa na damu sehemu mbali mbali za mwili ikiwemo puani, kwenye fizi, mdomoni na kwenye njia ya haja kubwa, na aina nyingine ni ile ambayo hutokana na shinikizo la damu ambalo hupatikana kwa kiwango cha chini.
“Ugonjwa huu mpya kwa Tanzania mlipuko wake umekuja wakati wa mvua za masika hivyo kuchangia kuongezeka kwa wagonjwa kutokana na mazalia kuongezeka,” alisema na kuongeza njia pekee ya kukabiliana nao ni kuhimiza usafi wa mazingira.

No comments: